The Rock City Mall ndiyo shopping mall kubwa kuliko zote Tanzania iliyopanda juu

NA DEREK MURUSURI
Mwanza

JENGO maridadi la The Rock City Mall linalolipamba Jiji la Mwanza, ndiyo “shopping mall’ kubwa kuliko zote nchini Tanzania kwa sasa, ambayo ina moja lililosimama kwenda juu.

The Rock City Mall, ni uwekezaji mkubwa wa dola za marekani milioni 40, takriban Shilingi bilioni 88 wakati huo, ni mradi mkubwa na unaoleta faida kubwa kwenye jiji la Mwanza na Kanda yote ya ziwa, shukrani kwa PSSSF na wabia wenza. Thamani yake kwa sasa inakaribia kuvuka Sh100 bilioni.
Uzuri wa ndani wa Rock City Mall, ni mithili ya Malls za Mataifa makubwa yaliyoendelea duniani. Wabia walizunguka kwenye mataifa ya Ulaya ili kupata “design.”

Si watu wengi huwa wanapenda kufanya utafiti. Wengi huwa wanaamini kila wanachokisikia tu bila hata kujisumbua kutafuta ukweli. Wengi wana taarifa zisizo sahihi kwa kuzingatia utamaduni huo. Hii ni hatari kwa biashara na kupata mafanikio bila utafiti ni bahati, utakosa fursa, utaambulia hasara tupu.

Tukiwa Sato Sangara, Mgahawa uliojizolea sifa kem kem katika eneo la nje hapo hapo The Rock City Mall, mkazi mmoja wa Jiji la Mwanza (jina ninalihifadhi), aliniambia, “hili jengo ni zuri lakini halina wapangaji kabisa.”

Wakati huo nilikuwa nimetoka kulitembelea jengo hilo na kupata takwimu sahihi kutoka kwa wakaguzi wa Serikali na kwa utawala wa jengo kuwa hadi tarehe 30 Juni, 2024, (miezi takriban minne tu iliyopita) jengo hili lilikuwa limejaa kwa asilimia 91. Wengi wana takwimu za wakati ule jengo limefunguliwa, wanatembea na takwimu hizo hadi leo. Wameganda nazo.
The Rock City Mall ya Mwanza, Tanzania. Shopping Mall hii inayotajwa kuwa kubwa kuliko zote nchini, iliyosimama pamoja (free standing), imeinua hadhi ya jiji la Mwanza, imetengeneza ajira, imeinua biashara, imeleta biashara ambazo awali hazikuwepo katika Jiji la Mwanza na Kanda ya Ziwa na hutembelewa na wanunuzi kutoka eneo la maziwa makuu na nje ya Afrika.

Maneno hayo anayathibitisha Meneja wa The Rock City Mall, Bi Annette Shoo. “Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2024, jengo letu lilikuwa limejaa kwa asilimia 91, wapo wanaoingia na pia wapo wanaotoka, kama ilivyo kwenye biashara ya majengo mahali pote lakini siku si nyingi, nafasi zitakuwa za kugombania, mahitaji yanaongezeka kila uchao na waweka nia ya kupanga wanaongezeka,” alisema.

Rock City Yatajwa Kuongoza Nchini

Bw. Willy Nkya wa Willy experience, yeye anautaja mradi huu kuwa ni mkubwa kuliko miradi mingine ya malls nchini Tanzania, zilizojengwa kama “one unit”.

Bw. Nkya anasema mradi huu wa The Rock City Mall unakaribiana na Westgate Shopping Mall, iliyoko katika Barabara ya Mwanzi, eneo la Westlands katika jiji la Nairobi, Kenya, ambayo inajinasibu kuwa ndiyo Shopping Mall inayoongoza kwa ukubwa na huduma katika Afrika Mashariki yote.

Ukubwa wa Eneo

Rock City Mall inayomilikiwa na Kampuni ya ubia ya Mwanza City Commercial Complex Company Limited, ina eneo lenye ukuwa wa mita za mraba 56,400, sawa na ekari 5.6.

Bi Annette Shoo anasema kuwa eneo la mita za mraba 47,000 limejengwa na sehemu ya kupangisha (rentable space) katika Mall hii kubwa nchini ni mita za mraba 22,000. Eneo lililobaki ni la maegesho ya magari na michezo ya watoto.

“Upo mradi mwingine tunakwenda kuuanza muda si mrefu,” anasema Meneja Annette Shoo ambaye ni Mtaalamu wa Milki za Majengo, mwenye uzoefu wa ndani na nje ya nchi.

“Ninaishauri PSSSF pamoja na wabia wenzake, wafikirie kujenga hoteli ya nyota 3 au 5 ambapo wageni kutoka duniani kote, wanaokuja kufanya mahemezi halafu wanakwenda kulala kwingine, ikiwa ni pamoja na watalii wanaokwenda Serengeti, wawe wanalala hapa hapa,” anasema mpangaji wa Rock City Mall, Bw. Robert Bugali.

Bw. Bugali aliyeanza na meza ya nje tu akiwa na mtaji wa shilingi 1.8mil, leo amepanga vyumba viwili ndani ya Rock City na mtaji wake umekuwa hadi 50m/- na hana mpango wa kutoka hapo.

Meneja Annette Shoo anakiri kuwa watalii wengi wanaopita Mwanza kwenda kwenye Mbuga maarufu na kubwa kuliko zote duniani ya wanyama ya Serengeti, hupata mahitaji yao mengi katika shopping mall hiyo ya Rock City, iliyolibadilisha kabisa jiji la Mwanza.

Eneo la The Rock City Mall, iliyoshikiliwa na nguzo mithili ya miguu ya twiga na katikati likiwa na lango mithili ya tezi za sato au sangara, limepakana na viwanja maarufu vya mikutano mikubwa vya Furahisha. Uwanja wa mpira wa CCM Kirumba pia hauko mbali sana.

Shopping more hii ni kimbilio la wana Mwanza katika siku za sikukuu. Viwanja vya jengo hilo hufurika watu na magari. Kadri utamaduni wa kupata vitu vizuri unavyozidi kukita mizizi miongoni mwa wana nzengo na hata mikoa ya Kanda ya Ziwa, ndivyo Menejimenti na Bodi ya The Rock City Mall inavyojiandaa kuongeza uwekezaji mkubwa zaidi.

Mikoa ya Kanda ya Ziwa ni ukanda wa madini. Kampuni za nje zenye wafanyakazi wenye mahitaji ya viwango vya kimataifa, hufurika kufanya mahemezi yao katika shopping mall hii ya Rock City. Ni uwekezaji wenye mahitaji (demand-driven investment).

“Zamani hapa tulikuwa tunajivunia NCU ambayo ndiyo ilikuwa na uwezo wa kujenga magorofa makubwa labda na Hospitali ya Bugando, siku hizi NCU yetu ni Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, hasa PSSSF. Tunawashukuru kwa mradi huu wa Rock City, nasisi Mwanza tunahesabika jamani,” anasema Thomas Ndoshi, mfanyabiashara wa magari.

Wafurahia Rock City Mall imewapaisha

Bw. Albert Girenga ni Mkurugenzi Mkuu wa Victory Auditors. Alikuwa amepanga kwenye jengo moja katikati ya jiji la Mwanza. Alisamehe kodi iliyokuwa imebaki ya miezi sita (6), akahamia Rock City Mall.
Mwandishi wa makala hii, Bw. Derek Murusuri (katikati), akiwa na wapangaji wa The Rock City Mall, aliofanya nao mahojiano, Bw. Abdallah Shija wa Sato Sangara (Kushoto) na Bw. Albert Girenga wa Victory Auditors.

“Nilitumia Sh7mil. kuiremba ofisi mpya lakini muda si mrefu, SNV wakatembelea ofisi zangu, nikapata kazi ya Sh42mil. Safari yangu ya mafanikio ikaanzia hapo,” anasema Bw. Girenga.

“Jengo au location ilinibeba. Hapa Rock City Mall ni matangazo tosha. Jengo linaitangaza biashara yako. Partners wangu kutoka Uholanzi walikuja moja kwa moja na baada ya kuona ofisi inaeleweka, wakanipa kazi,” aliongeza Bw. Girenga.

Bw. Girenga sasa amefungua kampuni ya uwekezaji kwenye soko la mitaji (CMSA), Equinvest Brokers Company Ltd. Kampuni hii mpya ni ya pekee ya hisa na mitaji katika Kanda ya Ziwa.

Naye Bw. Abdallah Shija Mtunga wa Sato Samaki, ambayo ni kama Samaki Samaki ya Dar es Salaam, anafurahia mafanikio ya uwekezaji wake na wenzie watatu miezi kumi tu katika jengo la Rock City Mall.
Rock City Mall nyakati za usiku, watu huja kwa starehe mbalimbali.

“Tunauza samaki wa ziwa viktoria kwa asilimia 100. Tunapata wageni mbalimbali kutokana na huduma nzuri ya chakula na vinywaji. Wageni wetu wanatoka ndani na nje ya nchi, kwa kweli location ni supportive,” anasema Bw. Shija, aliyewahi kufanya kazi kwenye mgahawa wa villa park, iliyokuwa katika eneo la CCM Kirumba, Mwanza.

Sasa hivi Bw. Shija na waliokuwa wafanyakazi wenzake wa Villa Park, ni waajiri na wamiliki wa mgahawa huo maarufu katika jiji la Mwanza, hasa kwa samaki choma wa Sato Sangara.

Wateja Takriban Elfu 10 Hutembelea Rock City Mall kila Siku

Ukiingia katika mahesabu ya Rock City Mall na ukaitembelea mchana na usiku ambapo takriban watu 10,000 huwapo katika jengo hilo kila siku, utaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuiruhusu LAPF, sasa PSSSF kufanya uwekezaji huo muhimu kwa Mwanza, Kanda ya Ziwa na Taifa.

Wa Mwanza Wakoshwa na Dkt. Samia Anavyofungua Uchumi

Daraja la juu la JPM la Kigongo Busisi la Mwanza litafungua njia kuu ya uchumi wa Mwanza, kwa mazao ya kilimo, uvumi na viwanda. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliapa kuwa mradi huo kwa wana Mwanza, lazima ukamilike, tena kwa wakati.

“Wana Mwanza wamekoshwa na ujenzi wa daraja refu, la juu ya maji na la kihistoria la Mwanza na ujenzi wa meli za MV Mwanza na MV New Victoria, tumekoshwa sana na Dkt. Samia, anafungua uchumi wa Kanda na nchi yetu. Kwa kweli tumefurahi mno,” anasema Costa Jidonge Masalu wa Ghana, Mwanza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akitembelea na kukagua ujenzi wa Meli ya MV Mwanza, Jiini Mwanza mwaka 2023.

Wabia wa Mradi

Mradi huu ambao Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSSSF) una unaumiliki kwa asilimia 90 pamoja na Jiji la Mwanza lina asilimia sita (6) na Halmashauri ya Ilemela ina asilimia nne (4), haujawahi kutengeneza hasara.

Kwa Mafanikio haya, PSSSF Wajenge Mall kama Rock City Dodoma

Kwa vile The Rock City Mall imeonesha kuwa na mafanikio makubwa, kwa kuhamasisha maendeleo ya biashara zingine, wananchi, kodi ya serikali, uzuri wa mji, sifa ya nchi na mengine mengi, sio vibaya PSSSF ikafikiria kuweka mradi mkubwa kama huo katika Jiji la Dodoma pia.

Mradi mkubwa wa aina hii, tena wa muda mrefu, mafanikio yake yataanza kupimwa kuanzia miaka 10 na kuendelea. Bi Annette Shoo alisema kuwa katika mwaka huu wa fedha, Wabia watakwenda kupata gawio lao ili kuanza kufaidi matunda ya uwekezaji wao.

Ikiwa Mradi huu utaongeza uwekezaji mwingine katika ujenzi wa hoteli ya kulala wageni ya nyota 3 au 5, The Rock City Mall itawavutia watalii na wageni wengi zaidi na kuongeza mapato yake maradufu. Kazi inaendelea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news