Tuendelee kuiombea nchi idumu katika amani-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza masheikh kutumia mikusanyiko ya kiimani kuiombea nchi amani ili Serikali iendelee na mipango ya maendeleo.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 25, 2024 alipofungua Ijitimai ya Sita katika Msikiti wa Fissabilillah Tabligh Markaz, Kidoti, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa bila ya kuwepo kwa amani, hakuna jambo linaloweza kufanyika na kufikia malengo ya nchi.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amewasisitiza viongozi, masheikh, na waumini wa dini ya Kiislamu kuendelea kuhubiri amani, maadili, na tabia njema ili kujenga jamii bora.

Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa ni jukumu la kila mmoja kusisitiza jambo hilo, na wala si la kuwaachia masheikh na maamiri pekee yao.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameipongeza Jumuiya ya Fissabilillah Tabligh Markaz kwa kuendeleza Ijitimai kwa mafanikio makubwa kila mwaka na kuahidi kuwa Serikali itaunga mkono juhudi hizo.

Kwa upande mwingine Rais Dkt. Mwinyi amewanasihi viongozi wa dini kutojiingiza kwenye siasa na mambo yaliyo nje ya misingi ya Uislamu.
Akitoa salamu za Jumuiya ya Kiislamu ya Fissabilillah Tabligh Markaz Zanzibar, Sheikh Kassim Saleh ameielezea hali ya amani nchini na kasi ya maendeleo iliyofikiwa Zanzibar kama matokeo ya kuwa na Rais mcha Mungu na anayejali watu wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news