Tuna akiba ya kutosha fedha za kigeni-Gavana Tutuba

NA GODFREY NNKO

AKIBA ya fedha za kigeni iliongezeka kufikia dola za Marekani milioni 5,413.6 mwishoni mwa Septemba 2024 kutoka dola za Marekani milioni 5,345.5 mnamo Juni 2024.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba ameyasema hayo kupitia taarifa aliyoitoa leo Oktoba 3,2024 kwa umma.

Ni wakati akielezea uamuzi wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania ambayo ilikutana Oktoba 2,2024.

Katika kikao hicho,MPC imeamua Riba ya Benki Kuu (CBR) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Disemba 2024.

"Akiba hii inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa zaidi ya miezi 4, ambayo inaendana na lengo la nchi.

"Upatikanaji wa fedha za kigeni unatarajiwa kuendelea kuimarika, kutokana na ongezeko la bei ya dhahabu kwenye soko la dunia, shughuli za utalii na mauzo ya bidhaa asilia kama korosho, tumbaku, kahawa na pamba.

"Mauzo ya mazao ya chakula hususan mahindi na mchele kwenda nchi jirani, pia yanatarajiwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni."

Wakati huohuo, Gavana Tutuba amesema, kupungua kwa uagizaji wa mbolea na kupungua kwa bei za bidhaa za mafuta ya nishati kunatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni.

"Vilevile, matakwa ya kisheria kuhusu kunukuu na kufanya malipo ya ndani kwa shilingi ya Tanzania yanatarajiwa kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni nchini na kuongeza ufanisi wa sera ya fedha."

Gavana Tutuba ameongeza kuwa,Benki Kuu itaendelelea kuimarisha akiba ya fedha za kigeni kupitia mpango wa ununuzi wa dhahabu katika soko la ndani kwa kutumia shilingi ya Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news