NA LWAGA MWAMBANDE
SIMBA Sports Club na Young Africans Sports Club ndizo klabu pekee nchini Tanzania na pengine Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zenye ushawishi na hamasa kubwa, kutokana na namna ambavyo zimejitengenezea mashabiki wake ambao bila utani na tambo, uwanjani huwa pamepooza.
Ukitaka kujua tambo na utani huo, siku ya Kariakoo Derby ndiyo utapata kuyafahamu kila maneno na vijembe ambavyo wala kwa mashabiki hao si karaha, bali ni njia moja wapo ya kuonesha mmoja kati yao ni mwenye nguvu zaidi.
Ni utani ambao licha ya kuanzia mitaani,majumbani, uwanjani pia huenda mbali zaidi kwa upande mmoja kuonesha udhaifu wa klabu moja, kuanzia usajili, makombe, nafasi ya klabu katika ngazi za kitaifa hadi Kimataifa.
Pia, utani huo wakati mwingine huwa unavuka mipaka zaidi kwa kuyagusa maslahi ya waliowekeza katika klabu hizo, huku mmoja akitaniwa mtaji wake ni mdogo, mwingine amejaza matangazo kwenye jezi na wakati mwingine fungu linalotoka kwa wawekezaji ni ndogo, haliendani na hadhi ya klabu.
Tambo na utani huo, ndiyo huwa unasababisha klabu hizo kuendelea kuwa na nguvu zaidi, kwa sababu wakati mwingine utani huwa unagusa hadi kwenye udhaifu wa mmoja wao. Licha ya utani huo kunogesha soka la vilabu hivyo,Mshairi wa Kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, siku za karibuni utani huo ni kama umepooza. Endelea.
1. Haya ni mabadiliko, yabidi tuyapokee,
Yameshatupa mwaliko, mbele na tuendelee,
Kurudi nyuma hakuko, ya kwamba tujitetee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
2. Utani Simba na Yanga, uache uendelee,
Kuunga hata kupinga, tukuache kutokee,
Ila tunavyojipanga, hivi sasa mambo chee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
3. Miye si mkongwe sana, ya kwangu nielezee,
Tumekuwa twapambana, ushindi utokezee,
Anoshindwa ni kununa, na nje asitokee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
4. Kwa wachezaji zamani, hapa niwaelezee,
Ni mapenzi ya moyoni, yalifanya wachezee,
Si hawa kina Yondani, huku huko watokee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
5. Fikiria Kibadeni, vipi Yanga achezee,
Na Manara wa zamani, vipi Simba achezee,
Upenzi likuwa ndani, kwamba wapi wachezee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
6. Likuwa nadra sana, mchezaji atokee,
Simba awe bora sana, kisha Yanga achezee,
Japo hao twawaona, kumbukumbu zipotee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
7. Twamjua Zamoyoni, ni wapi atokezee,
Kwenye kamati za ndani, mipango aelezee,
Anaonekana duni, kwamba kote achezee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
8. Kuwa ndumilakuwili, acha tukupotezee,
Kokote hawakujali, acha wakupotezee,
Kama mtu wa madili, ndivyo tukuelezee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
9. Pesa kushika hatamu, na hata nielezee,
Utani siyo mtamu, uwanjani upotee,
Ubakie kwetu humu, kutamba tuendelee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
10. Kucheza toka moyoni, ni nani umwelezee,
Timu haiko moyoni, ni vipi aitetee,
Aingia uwanjani, mshahara apokee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
11. Sasa kama kawaida, hamahama itokee,
Leo huku Simba kada, vizuri aichezee,
Dau lije kama ada, na Yanga apotelee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
12. Karibia kila mwaka, ni hamisho zitokee,
Pesa nguvu zimeshika, na utani uozee,
Wale wanataabika, mashabiki wazoee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
13. Wachezaji wa kigeni, kushuka wakuchochee,
Wanachowaza mapeni, kotekote wachezee,
Mashabiki uwanjani, kulia waendelee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
14. Sasa inawezekana, hadi timu itokee,
Wahamaji wengi sana, timu hizi wachezee,
Ni kawaida waona, kokote watokezee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
15. Na nyie wahafidhina, mlivyo muendelee,
Utani tunaoona, zidisheni mchochee,
Hali halisi mwaona, uache uteketee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
16. Pesa ndizo zinasema, maisha yaendelee,
Manenoneno yakwama, kusema tuendelee,
Pesa zitazidi vuma, mbele na tuendelee,
Utani Simba na Yanga, ni kama umepooza.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602