Vijana wa Kitanzania waonesha bidii bunifu Akili Undwe na Roboti,Dkt.Mwasaga atoa neno

NA DIRAMAKINI

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya TEHAMA Tanzania (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema, anaona fahari kubwa, kushuhudia namna ambavyo vijana wa Kitanzania wanaonesha bidii katika bunifu mbalimbali ambazo zinahusiana na Teknolojia ya Akili Undwe na Roboti nchini.
Dkt.Mwasaga ameyasema hayo leo Oktoba 23, 2024 wakati wa mahojiano na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1) akielezea maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini.

Mahojiano hayo yamefanyika ikiwa ni siku chache zimepita baada ya Kongamano la Kihistoria la TEHAMA Tanzania ambalo lilifanyika kuanzia Oktoba 13 hadi 17, 2024 na kutamatika kwa kishindo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar e Salaam.

Pia,amesema waifanikiwa kuandaa Kongamano la Mwaka la TEHAMA Tanzania ambalo lilikuwa na sura ya Kiafrika huku likijumuisha maonesho na mashindano ya Afrika kwa Akili Unde na Roboti kwa mafaniko makubwa kutokana na ushirikiano waliopata kutoka wizarani.

"Tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu wizara yetu ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ilifaya kazi vizuri sana na sisi ili kuhakikisha jambo letu linaenda vizuri.

"Katika kitu ambacho kinanipa furaha, vijana wa Kitanzania wana uwezo mkubwa sana kwa sasa hivi na wanajituma,"

Amesema, kwa sasa vijana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanafanya utafiti wa Roboti ambaye atakuwa na uwezo wa kufanya shughuli nyingi,

"Kwa hiyo, walichoamua kufanya wameanza kwanza na kichwa cha Roboti, kukifanya kwanza kiweze kuona, kutambua, na kuanza kuzungumza na wewe.

"Sasa, ili uweze kumfanya Roboti aweze kuzungumza kama mimi ninavyofanya na wewe hapa, kuna vitu viwili ambavyo vinatakiwa vitengenezwe, kimoja wapo ndiyo faida ya kongamano hili tulilolifanya.

"Katika kongamano hili tumeweza kuingia makubaliano na Kampuni ya nchini Italia ambayo tutatengeneza Mfumo wa Kiswahili ambao utawezesha Roboti yoyote duniani kuzungumza Kiswahili.

"Kwa sababu maroboti mengi unaona yanazungumza Kiingereza vizuri, kwa kuwa wametengeneza huo mfumo (Foundation Models), sasa hivi tumeingia makubaliano ya kutengeneza ya Kiswahili.

"Sasa, ukishatengeneza ya Kiswahili, roboti kama yule unamfanyia utafiti, akishawekewa ile foundation models yaani huo mfumo, sasa anakuwa anaweza kufikiria kwa haraka na akazungumza kama kawaida kama tunavyozungumza sisi."

Tume ya TEHAMA ilisaini makubaliano na Almawave ya nchini Italia siku ya Oktoba 16, 2024 ambapo ushirikiano huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya katika Sekta ya TEHAMA nchini.

"Kwa hiyo, haya mambo yote ni ya kitafiti na ndiko tunakwenda huko, yule ukisema azungumze kwa Kiingereza inakuwa ni rahisi tu, kwa sababu hiyo kazi tayari walikwishaifanya."

Dkt. Nkundwe Mwasaga akifafanua kuhusu Akili Undwe amesema kuwa, "Hili jambo ni vizuri nilielezee vizuri na kwa upana ili lieleweke vizuri kwa sababu tumekuwa tukitumia maneno mengi, kwanza tulianza na Akili Bandia, ikaja Akili Mnemba sasa hivi Akili Undwe, kwa hiyo hivyo vyote vinazungumzia Artificial Intelligence.

"Hii teknolojia, kinadharia ilianza siku nyingi,kuna watu walikuwa wanaona kabisa hizi mashine tunazozitengeneza duniani,zinaweza zikapewa uwezo wa kuweza kufikiri na kufanya mambo fulani, na ilianza miaka ya 1947 huko, ndiyo watu walikuwa wanafikiria kwamba tunatengeneza mashine, mashine zinaweza zikatusaidia kutusaidia kufanya kazi na inaongezewa tija.

"Lakini, tunaweza kuzipa uwezo mkubwa,sasa ili kuweza kuifanya mashine iwe na uwezo mkubwa wa kufikiria kama binadamu, kuna vitu vitatu vinahitajika, cha kwanza mashine inahitajika iwe na uwezo wa kuchakata taarifa.

"Cha pili, inatakiwa iwe na mfumo kwa Kiingereza tunaita Logarithm, mifumo ambayo inawezesha mashine kufanya shughuli fulani kwa kufuata utaratibu fulani, kuanzia mwanzo mpaka mwisho.

"Lakini, kikubwa zaidi iwe na taarifa za kutosha nyingi,sasa ukiangalia ile miaka ya 1947 huko ilivyokuwa inaenda vile vitu vya kwanza viwili, vilikuwa vipo,

Uwezo mkubwa wa kuchakata ilikuwa inawezekana, kutengeneza mfumo fulani (Logarithm) wa kufuata utaratibu fulani mpaka inamaliza kwa maana ya kuanza kazi mpaka inamaliza, hiyo ilikuwa siyo shida.

"Kitu kilichokuwa kinaleta shida ni kupata taarifa (data), sasa miaka yote hiyo ilikuwa zinafanyika tafiti, kuna kipindi fulani ziliisha, lakini sasa hivi tumepata bahati,hivyo vitu vitatu vyote vipo.

"Kwamba, tuna uwezo mkubwa wa kuchakata hata tukiangalia simu zetu,zina uwezo mkubwa sana wa kuchakata.Hiyo mifumo ambayo inaweza kufanya kazi kuanzia mitandao ya kijamii, sasa hivi kuna intaneti ya vitu vingi (The Internet of Things),tuna sensors nyingin za kutosha, kwa hiyo tunapata taarifa nyigi za kutosha.

"Kwa hiyo, kwa sababu hivyo vitu vitatu vipo kwa sasa, mashine zimekuwa na uwezo wa aina fulani ya kufikiria ambao huo uwezo zamani alikuwa nao binadamu peke yake."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news