LINDI-Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Twende Pamoja AMCOS,Zamoyoni Haji Mmango na Rajab Rashid Ngaigara ambaye ni Katibu wa Chama cha Msingi Twende Pamoja AMCOS wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kughushi nyaraka.
Wawili hao, Septemba 30,2024 wamefunguliwa Kesi ya Jinai Namba 27817/ 2024 dhidi ya Jamhuri katika Mahakama ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi mbele ya Mhe.Makwaya C. C ambaye ni Hakimu Mfawidhi Mahakama ya wilaya hiyo.
Washitakiwa wanakabiliwa na kosa moja kwa mujibu wa hati ya mashtaka ambalo ni Kughushi nyaraka kinyume na kifungu cha 333, 335(a) na 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu [Sura ya 16, Marejeo ya Mwaka 2019].
Aidha, washitakiwa kwa tarehe tofauti tofauti kati ya tarehe 9, Machi 2022 na tarehe 11, Aprili, 2022 katika Kijiji cha Kitogoro wilayani Liwale Mkoa wa Lindi kwa pamoja na kwa nia ovu ya kuhadaa, walighushi nyaraka ya shilingi milioni 10,000,000.
Nyaraka hiyo ilikuwa na kichwa cha habari “ Muhtasari wa Mkutano Mkuu wa Chama Uliofanyika tarehe 09.03.2022" kana kwamba nyaraka hiyo ni halali na imeidhinishwa kwenye kikao kwa ajili ya mkopo jambo ambalo washitakiwa walifahamu kuwa sio kweli
Washitakiwa wote wawili wamekana mashitaka dhidi yao. Aidha, washitakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti yaliyotolewa na Mahakama.
Kesi imepangwa Oktoba 21,2024 kwa ajili ya kusikiliza hoja za awali na kuanza kusikilizwa.Kesi hii inaendeshwa na Mwendesha Mashitaka,Joseph Japhet Emanuel wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Lindi.