Wahitimu Shule ya Sekondari Bethsaida wafundwa

DAR-Wahitimu wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Bethsaida wametakiwa kuendelea kuwa waadilifu na kuwa mfano mzuri katika jamii, huku wakisisitiza kuwa ni jukumu lao kuimarisha maadili na ujuzi waliyopata shuleni.Wito huo umetolewa leo Oktoba 19, 2024 katika Mahafali 16 ya shule hiyo iliyopo Mbezi Mpiji Magoe jijini Dar es Salaam na Constantine Kaniki ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo.

Amesema kuwa, kutokana na changamoto ya ajira nchini, wanafunzi wanatakiwa kufahamu na kujiandaa kutafuta fursa za kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa pindi watakapomaliza masomo yao.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa elimu kama daraja kuelekea mafanikio, huku akiwasisitizia wahitimu kuwa mafanikio hayaji kirahisi na yanahitaji juhudi na ubunifu.
Pamoja na hayo amewapongeza viongozi wa shule hiyo kwa kukaa na kuamua kuokoa maisha ya watoto , hasa hawa wa jinsia ya kike ambao mara nyingi ndio wanaoangukia kwenye kundi la waathirika wa matukio.

"Ni watoto wengi sana wanaachwa wakitaabika mitaani bila msaada, na kwa hatua hii mliyochukua ya kuanzisha hiki kituo na shule, na kwa hatua mliyofikia ikiwemo mafanikio ya kielimu kwa wanafunzi wanaopitia shule tokea ilipoanzishwa. Hivyo mnapaswa kupewa pongezi kubwa sana,"amesema.
Amewapongeza taasisi za dini, wahisani na wafadhili, pamoja wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa michango yao ambayo inaiwezesha shule hiyo kutekeleza majukumu yake katika nyanja za ufundishaji na kutoa huduma ya kuyanusuru maisha ya watoto hao.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Holliness Mushi amesema, lengo la kuanzishwa kwa shule hiyo lilikuwa ni kuipunguzia serikali mzigo mkubwa wa watoto yatima au wale wanaoishi katika mazingira magumu kwa lengo la kuwapatia elimu bora kama ilivyo kwa watoto wengine.

"Lengo la kuanzisha shule hii pia ni kupunguza uwezekano wa kufanyiwa vitendo vya ukatili majumbani na mitaani watoto wa namna hii; mfano ubakaji, kunyimwa haki zao za msingi ambapo hapa tunawaanda kuwa watu bora, wazalishaji na wenye thamani katika jamii na pia wenye kujiamini,"amesema.
Amesema,ufaulu wa wanafunzi umezidi kukua kwani mwaka jana asilimia 90 yaani 26/29 walijiunga na masomo ya kidato cha tano na wengine walijiunga na vyuo vya kati. Hakukuwa na mwanafunzi aliyefeli kwa kupata zero.

Amesema,kwa mwaka huu 2024, wanafunzi wote walipata division I, II, na III tu, hakukuwa na Four wala zero katika mtihani wa mock wa kidato cha nne.

"Tunajivunia matokeo ya watoto wetu kwani yanatokana na juhudi zao pamoja na kazi nzuri inayofanywa na timu ya waalimu wetu. Karibu kila mwaka angalau asilimia tisini (90%) ya wanafunzi wote wanaomaliza kidato cha nne huchaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano ama vyuoni,"ameeleza.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Shule ya Sekondari ya Bethsaida, Raymond Machary amewatia moyo wahitimu hao kwa kuwaambia wanapoelekea katika mitihani yao ya mwisho wasiwe na woga bali wajiandae vizuri ili kesho yao waweze kuwasaidia wazazi.

Aidha,Machary amewaomba wazazi kuwa sehemu ya faraja kwa watoto hao na kuwasaidia katika nyanja zote ikiwemo ya kiuchumi kwani kufanya hivyo watasaidia kukidhi mahitaji yao.
"Tunaamini mnaweza lakini chochote ambacho mtakuwa mmebarikiwa na mwenyezi Mungu mkitoa katika fungu la kumi mtabarikiwa na Mwenyezi Mungu,"amesema.

Shule ya Sekondari Bethsaida ambayo ni ya wasichana hususani wale ambao ni yatima na ambao wazazi wao hawajiwezi ilianza kama kituo cha kulelea watoto yatima mwaka 2005 na hatimaye kuwa shule ya upili mwaka 2006, ambapo mpaka sasa ni Mahafali ya 16 na kwa mwaka huu 2024 wahitimu 35 wamehitimu masomo ya kidato cha nne.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news