MWANZA-Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza imemhukumu aliyekuwa wakala wa kukusanya mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe,Fred Chamata Salum adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Ni baada ya kukutwa na hatia katika makosa ya ufujaji na ubadhirifu pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na vifungu vya 28 (1) pamoja na 31 vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [CAP 329 R.E 2022].
Vikisomeka pamoja na Aya ya 21, Jedwali la kwanza, pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) na (3) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 kama ilivyofanyiwa Marejeo Mwaka 2022.
Hukumu dhidi ya Bw. Fred Chamata Salum imetolewa Oktoba 9, 2024 kutokana na Shauri la Uhujumu Uchumi Na. 06/2023 lililokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Lucas Nyahenga.
Shauri ambalo liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza,Bw. Moses Malewo.
Awali ilielezwa kuwa Mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo kwa mashtaka tajwa hapo juu kwa kushindwa kuwasilisha kiasi cha shilingi 16,245,550 katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe.
Ni fedha ambazo alizikusanya kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato vya Halmashauri hiyo akiwa wakala wa kukusanya mapato.
Na kwamba Bw. Fred Chamata Salum alifanya hivyo akijua ni kinyume na Memoranda ya Fedha za Halmashauri za Mwaka 2009, lakini pia Kinyume na Sheria ya Fedha za Halmashauri sura ya 290 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Sheria hizo zote zilimtaka kila alipokusanya mapato ya halmashauri kuyawasilisha kwenye akaunti za halmashauri kila siku anapokusanya ama kesho yake endapo kuna changamoto.
Sambamba na kifungo cha miaka 20 jela, ametakiwa pia kurejesha katika Halamashauri ya Wilaya ya Ukerewe kiasi cha shilingi 16,245,550.
Tags
Habari
Mahakamani Leo
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU
TAKUKURU Tanzania