Walimu wa madrasa wana mchango mkubwa kuboresha maadili katika jamii-DC Said

ZANZIBAR-Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Unguja,Mheshimiwa Hamid Seif Said amesema, walimu wa madrasa wana mchango mkubwa katika kuboresha misingi bora ya maadili katika jamii.
Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya walimu wa madrasa wanachama wa Wilaya ya Kaskazini "B" katika ukumbi wa Madrasa Mahonda Msuka.

DC huyo amesema, walimu wa madrasa mchango wao wa kuwapatia watoto elimu ya akhera ni mkubwa ambao unasaidia katika makuzi yao.

Amesema, endapo elimu ya madrasa itatumiwa ipasavyo changamoto nyingi zinaweza kuepukika katika jamii ikiwemo vitendo vya udhalilishaji.

Ameeleza kuwa, ikiwepo jamii yenye kuzingatia maadili katika kuwalea watoto kupitia misingi ya dini itasaidia kupata watoto wema na wenye tabia njema.

Aidha, amewataka walimu hao kutovunjika moyo katika utendaji kazi wao pamoja na kutumia hekma katika ufundishaji ili kuiweka nchi katika amani.
Vile vile ameahidi kuviunganisha vyuo vya madrasa ambavyo havijakamilisha usajili ili kuweza kujiunga na jumuiya hiyo ili kuvisaidia madrasa hizo.

Hata hivyo, amesema atawashirikisha walimu wa madrasa na maafisa elimu wilaya katika kufanya maamuzi ya kutenga muda wa kupatia wanafunzi muda wa kujifunza elimu ya Dini kupitia madrasa.

Kwa upande wake Naibu Katibu wa Jumuiya ya Mtandao wa Vyuo vya Qur-an Wilaya ya Kaskazini "B", Foum Suleiman Juma amesema mafunzo hayo yatawasaidia walimu wa madrasa kuweza kusimamia majukumu yao ya ufanyaji kazi kwa uadilifu kwa kufuata miongozo na maamrisho ya Mwenyezi Mungu (s.w).

Amewaeleza kuwa endapo walimu wa madarsa watakuwa wakweli katika kusimamia miongozo ya dini katika kupambana na kila maovu na kutangaza yaliyomema itasaidia nchi kupambana na maovu.

Nao washiriki wa mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kuwaweka pamoja walimu wa madrasa ili kuweza kuhamasisha jamii katika kuwepo malezi shirikishi na kuipeleka mbele Dini ya Kiislam.

Aidha,amewataka wazazi na walezi kuendeleza ushieikiano katika malezi ya watoto kupata jamii yenye maadili mema.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Mtandao wa Vyuo vya Qur-an Wilaya ya Kaskazini B kwa lengo la kuviweka pamoja vyuo vya madrasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news