Waliosoma Milambo wamtunuku mwalimu wao Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere tuzo maalum

MARA-Umoja wa Wanafunzi waliosoma Shule ya Sekondari Milambo iliyoko mkoani Tabora (AMSHA) wamezindua zawadi ya mwalimu bora wa mwaka kwa shule hiyo.
Kwa mwaka huu tuzo hiyo imetolewa kwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwalimu Nyerere alifundisha katika Shule Sekondari Milambo wakati huo Ikiitwa St. Mary's Secondary School kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa jina la Mtemi wa Wanyamwezi, Milambo.
Uzinduzi wa tuzo hiyo umefanyika kijijini Mwitongo, Butiama mkoani Mara alikozaliwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na tuzo kukabidhiwa kwa mtoto wa sita wa Mwalimu, Godfrey Madaraka Nyerere.

Kwa mujibu wa Mjumbe wa Bodi ya AMSHA, Abdul-Razak Badru, mshindi atakuwa akipewa zawadi na fedha taslimu na kwa mwaka huu wamemtunuku Hayati Mwalimu Nyerere.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, amewapongeza waliosoma Milambo kwa kuwaenzi walimu na kuamua kuwapa tuzo kwa mara ya kwanza.

"Vijana hawa wametambua mchango wa Walimu ulioiwezesha Tanzania kufika hatua hii. Na wakawiwa kutoa Tuzo Maalum kwa familia ya Baba wa Taifa (Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere) kwa ajili ya kutambua mchango wake kama Mwalimu, lakini kama kiongozi mkuu wa nchi yetu aliyepambana pamoja na wazee wengine kuhakikisha Tanzania inakuwa huru.

"Lakini, aliyepambana kuhakikisha maendeleo tunayoyaona leo msingi wake aliuasisi yeye.

"Mimi kwa nafasi yangu kama Mbunge wa Butiama, lakini Naibu Waziri Katiba na Sheria ninafaka pia kwamba Waziri wangu Mheshimiwa Pfofesa Paramagamba John Haidadi Mwaluko Kabudi kuwa ni mmoja wa vijana wakati huo aliyesoma palepale Milambo.

"Kwa maana hiyo, naye ni mazao ya watu ambao walifundishwa na Baba wa Taifa, japo alifundisha kwa miaka mitatu."
Tuzo hiyo imetolewa kipindi hiki ambapo Taifa litaadhimisha Kumbukizi ya miaka 25 tangu kufariki dunia kwa Mwalimu Nyerere ambapo kilele chake ni Oktoba 14.

Godfrey Madaraka Nyerere ambaye ni mtoto wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye aliyepokea tuzo ya hiyo kwa niaba ya familia.

Godfrey ameishukuru na kuipongeza AMSHA kwa kuja na wazo hilo.

"Nitoe shukurani za dhati kwa AMSHA na uongozi wa AMSHA kwa kupata hili wazo la kuzindua tuzo hii na kuamua Mwalimu Nyerere yeye ndiye awe wa kwanza kupata tuzo hii."
Amesema, wao kama wanafamilia wanapoona jambo kama hilo ambalo linaendelea kumuezi Hayati Baba wa Taifa inakuwa ni faraja kubwa kwao.

Pia, amesema zawadi alizopokea kwa niaba ya Mama wa Taifa, Maria Nyerere ambaye yupo jijini Dar es Salaam ikiwemo tuzo ataziwasilisha pia katika Makumbusho ya Mwalimu Nyerere ili wengi waendelee kujifunza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news