Wanahabari watano waibuka kidedea Tuzo za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)

DAR-Mwenyekiti wa Bodi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari amewatunukia rasmi tuzo waandishi wa habari waliofanya vizuri kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2023 hadi Juni 2024 katika kuandika habari za hali ya hewa nchini.
Hafla hiyo fupi ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, tarehe 28 Oktoba 2024.

Kabla ya kukadidhi tuzo hizo kwa washindi, Mhe. Mshibe ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo aliipongeza TMA kwa kuendelea kuwashirikisha na kutoa motisha kwa wanahabari katika utoaji elimu na usambazaji wa huduma za hali ya hewa nchini.

Alieleza kuwa, TMA ni moja ya taasis chache nchini, zinazothamini mchango wa wanahabari kwa ujumla ikiwemo ubunifu wa kuanzisha TUZO ya wanahabari bora wa habari za hali ya hewa nchini kwa miaka mitano sasa, ambapo kwa mwaka huu nimeelezwa kuwa TMA imeongeza wigo wa washindi.
“Katika kuhakikisha tuzo hizi zinaendelea kuwa bora zaidi, mwaka huu Mamlaka imeboresha maeneo kadhaa ikiwemo kuongeza vipengele viwili vya waandishi kutoka nje ya Dar es Salaam na Zanzibar pamoja na kuboresha zawadi za washindi, hongereni sana TMA.

“Lengo kuu la Tuzo hizi ni kuendelea kuleta hamasa na kujenga umahili katika uandaaji na usambazaji wa tarifa za hali ya hewa kwa jamii, na kuimarisha mchango wa wanahabari katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa,” alieleza Dkt.Mshibe.

Akimkaribisha mgeni rasmi kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA, Dkt. Hamza Kabelwa, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri alisema Mamlaka kwa kutambua mchango huu mkubwa, imeendelea kuimarisha mahusiano haya kwa kuendelea kutoa motisha mbalimbali kwa wanahabari ikiwemo kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa takribani miaka 15 sasa hususani kipindi cha maandalizi ya utabiri wa mvua za misimu.
“Mafunzo haya yamekuwa yakitolewa, vilevile, kutafuta fursa za ushiriki wa waandishi wa habari kwenye mafunzo au majukwaa ya kimataifa mfano;

"Mwaka jana waandishi wa habari 10 walipata mwaliko wa kushiriki mafunzo Nairobi, Kenya (wengi wao wapo katika kundi hili) na mwaka huu mmoja wao aliweza kushiriki katika kongamano la kuaandaa utabiri wa msimu wa Vuli 2024 kwa nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika nchini Kenya, na huko nyuma wapo walioshiriki katika makongamano hayo Adis Ababa, Ethiopia na Entebe, Uganda,” ameeleza Dkt. Kabelwa.
Hafla hiyo ilifanyika wakati wa warsha ya wanahabari katika kujadili utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka (Novemba 2024 hadi Aprili 2025).

Washindi wa tuzo hizo walikuwa; Mshindi wa TV na Redio ni John Mathias kutoka TBC 1, mshindi wa Zanzibar ni Othman Ali Juma kutoka Alnoor FM,mshindi wa mikoani ni Adam Hando kutoka CG FM-Tabora, mshindi wa magazetini ni Superious Ernest kutoka gazeti la Uhuru na kwa mitandao ya kijamii ni Zaituni Mkwama kutoka Dailynews Digital TSN.

TMA inatarajia kutoa rasmi utabiri wa mvua za Msimu siku ya Alhamisi, tarehe 31 Oktoba 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news