Wananchi jitokezeni kugombea nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa-Mchengerwa

NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka wananchi wenye sifa za kugombea nafasi za uongozi wa Serikali za Mitaa, kujitokeza kuchukua na kurudisha fomu kuanzia tarehe 26 Oktoba hadi tarehe 1 Novemba, 2024 ili waweze kutimiza haki yao ya kikatiba ya kugombea katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Waziri Mchengerwa ametoa wito huo kwa watanzania wenye sifa, wakati akitoa tathmini ya uandikishaji wa wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mara baada ya kujiandikisha katika kituo cha Michikichini Kijiji cha Umwe Kaskazini Wilayani Rufiji.

“Zoezi la kuchukua na kurudisha fomu litafanyika kwa siku zote hizo kuanzia Oktoba 26 hadi Novemba 01, 2024 na kuongeza kuwa, muda wa kampeni utakapofika zifanyike kampeni za kistaarabu ambazo zitadumisha hali ya utulivu na Amani nchini,” Mhe. Mchengerwa alisisitiza.

Waziri Mchengerwa amewashukuru wananchi wote, wanachama na wapenzi wa vyama vyote vya siasa kwa kuendelea kuonesha ukomavu wa kisiasa kwa kufanya siasa za kistaarabu, siasa za hoja na si za ugomvi mpaka zoezi la uandikishaji likifikia ukomo.

“Niwasihi tuendelee kufanya siasa za kistaarabu na ninawakemea vikali wanaotaka kuleta siasa za ugomvi ambazo zinaweza kuhatarisha amani na utulivu tulionao katika taifa,” Mhe. Mchengerwa ameeleza.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amevisihi na kuvitaka vyombo vya dola viendelee kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kuwepo katika kipindi chote cha mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Sanjari na hilo, Waziri Mchengerwa amewasisitiza wasimamizi wa uchaguzi na wadau wote wa Uchaguzi wa Seriksali za Mitaa kuendelea kuzingatia Sheria na Kanuni za Uchaguzi, ili mchakato mzima wa uchaguzi uendeshwe kwa kuzingatia misingi ya Sheria na Kanuni zilizowekwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news