MANYARA-Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amezitaka kamati za pembejeo za wilaya kwa kushirikiana na wenyeviti wa wilaya kuhakikisha wakulima wanajisajili kwenye daftari la mkulima na wale waliojiandikisha msimu uliopita wanahuisha taarifa zao ili wasipitwe na fursa ya mbolea za ruzuku.
Sendiga ametoa wito huo Oktoba 10, 2024 alipokuwa akifungua maonesho ya siku nne yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ( TFRA) kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Oktoba, duniani kote.



Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent amesema, kupitia maonesho hayo wakulima na wananchi watapata fursa ya kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea pamoja na maeneo mengine yatakayowasaidia kuongeza uzalishaji.
Amesema, mbolea ni moja kati ya pembejeo muhimu zinazohitajika katika uzalishaji wa mazao, wakati mbegu bora zikichangia takribani asilimia hamsini ya uzalishaji wa mazao mbolea huchangia kati ya asilimia ishirini hadi arobaini na asilimia zinazobaki hutokana na uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo kwa jumla.