DODOMA-Watu zaidi ya milioni 1.6 wamehudumiwa kwenye kliniki za kutoa huduma za macho kwa mwaka 2023, kati ya hao asilimia 42 waliopata huduma walikuwa na umri chini ya miaka 15 huku asilimia 6 ya watoto hao wakiwa wenye ulemavu wa kutokuona. Hayo yameelezwa Oktoba 9, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dkt. Hamad Nyembea akimuakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama(Mb), wakati akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Macho Duniani yaliyofanyika katika kituo cha Afya Makora jijini Dodoma, kauli mbiu ikiwa “Penda Macho yako, Muhamasishe Mtoto kupenda Macho yake.”Dkt. Nyembea amesema, miongoni mwa vyanzo vikubwa vya matatizo ya macho kwa watoto na vijana ni mzio, upeo mdogo wa macho kuona unaorekebishika kwa miwani na majeraha kwenye macho.
“Matatizo ya macho yanaweza kusababishwa na mtoto wa jicho kwa 10% makengeza kwa 1.5%, makovu kwenye kioo cha jicho 1.1% na vidonda kwenye vioo vya jicho 1.5%, ugonjwa wa surua, upungufu wa vitamini A na saratani ya macho. Sababu hizi zote zinaweza kuepukika au kudhibitiwa endapo tutachukua hatua stahiki mapema,”amesema Dkt. Nyembea.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imeimarisha huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali za Rufaa za Kanda KCMC na Bugando ambapo kwa mwaka 2023, jumla ya watoto 631 sawa na asilimia 24.5 ya wahitaji wa huduma hizi walipatiwa huduma za upasuaji wa mtoto wa jicho na kupatiwa miwani.
“Ili kupanua wigo, Serikali imeongeza huduma hizi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma, lengo likiwa ni kufikia angalau asilimia 50 ya wahitaji wote ifikapo mwaka 2030, aidha, Serikali imekuwa ikifanya kambi maalum za uchunguzi na matibabu ya kibingwa na Ubingwa Bobezi ili kuongeza kasi katika kuwahudumia wananchi katika maeneo yao na kupunguza gharama za kusafiri umbali mrefu kuzifuata huduma hizi,” ameongeza Dkt. Nyembea.
Ametoa rai kwa jamii kuhakikisha inawalinda watoto kwa kuwaepusha na vitu vinavyoweza kuhatarisha afya zao za macho ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda wanaotumia kwenye runinga, simu pamoja na kompyuta.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyo ambukiza, Dkt. Omari Ubuguyu ameeleza kuwa huduma ya macho imeanza kutolewa tarehe 4 hadi 10 Oktoba, 2024 katika kituo cha Afya Makole na kauli mbiu ya mwaka 2024 imelenga zaidi kwa watoto na vijana lengo likiwa ni kuwahamasisha kupima na kupewa huduma za matibabu na kuongeza kuwa muitikio ni mzuri kwani zaidi ya mikoa 15 imefikiwa katika upimaji wa macho na wananchi wapatao 450,000 wamepimwa macho.
Akitoa salamu kwa niaba ya wadau wa macho, Bw. Edwin Barongo ambaye ni Afisa Mradi kutoka Shirika la Sightsavers wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa mchango wa kuhakikisha utoaji wa huduma bora za macho Tanzania na kuhakikisha huduma za MKOBA zinawafikia wananchi hususani jamii za vijijini ambako hakuna huduma za kibingwa pamoja na kusaidia kusomesha wataalam ili kuongeza nguvu kazi ya huduma za afya ya macho.