HELSINKI-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Finland, Mhe. Alexander Stubb.
Mazungumzo hayo yamefanyika kwenye makazi ya Rais jijini Helsinki leo Oktoba 10, 2024.
Wakati wa mazungumzo hayo, viongozi hao walijadiliana masuala ya ushirikiano na uhusiano yenye manufaa kwa pande zote mbili.
Viongozi hao walikiri kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Finland ulioanza tangu miaka ya 60 ni mzuri na hakuna budi kuenziwa na kuimarishwa zaidi ili kuendelea kuleta manufaa kwa mataifa hayo.
Aidha, Waziri Kombo alitumia fursa hiyo pia kuwasilisha salamu za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo alisema Rais Samia anashukuru kwa misaada ya maendeleo ambayo Finland imekuwa ikiipatia Tanzania. Amesema misaada hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa makundi yote nchini na hasa wananchi wa kawaida.