Waziri Dkt.Nchemba afungua Mkutano wa SADC-CISNA, asema Tanzania imepiga hatua huduma ndogo za fedha

NA GODFREY NNKO
Zanzibar

WAZIRI wa Fedha,Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa katika udhibiti wa huduma ndogo za fedha kwa ustawi wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba akimkaribisha Mheshimiwa Ali Suleiman Ameir, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu Zanzibar alipowasili kufungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba.

Ameyasema hayo leo Oktoba 1,2024 kupitia hotuba iliyosomwa na Mheshimiwa Ali Suleiman Ameir, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, Zanzibar.

Ni katika ufunguzi wa Mkutano wa 47 wa Mwaka wa Kamati ya Mamlaka za Usimamizi wa Bima,Masoko ya Mitaji na Huduma za Fedha zisizo za Kibenki (CISNA) jijini Zanzibar.

Kamati hiyo ipo chini ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). "Tumeshuhudia pia maendeleo makubwa katika udhibiti wa huduma ndogo za fedha kulikotokana na jitihada mbalimbali za Serikali ikiwemo kutungwa kwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018.
"Pamoja na kanuni zake za mwaka 2019 na kuimarishwa kwa mchakato wa upatikanaji wa leseni kwa watoa huduma ndogo za fedha."
Jambo lingine, Waziri Dkt.Nchemba amesema, ni kuanzishwa kwa mifumo ya usajili wa kidijiti wa vikundi vya msingi vya kijamii.

"Wakati ambapo mamlaka ya kutoa leseni kwa taasisi za huduma ndogo za fedha iko chini ya Benki Kuu ya Tanzania.

"Utoaji leseni kwa vikundi vya huduma ndogo za fedha vya daraja la 3 (SACCOS) umekasimishwa kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania na vile vya daraja la 4 ambavyo ni vikundi vya kijamii, umekasimishwa kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa."

Pia, Waziri Dkt.Nchemba amesema, usajili wa vikundi vya kijamii unafanywa kwa njia ya mtandao ikiwa ni pamoja na kupitia simu za mkononi.
Amesema,kutokana na hatua hizo, hadi kufikia Juni 30, 2024 jumla ya idadi ya watoa huduma ndogo za fedha waliosajiliwa katika madaraja yote matatu ilikuwa zaidi ya 56,000.

"Tunapoendelea kutekeleza Mpango wa Tatu wa Huduma Jumuishi za Fedha 2023/24 – 2027/28, urasimishaji wa huduma za fedha utaendelea kuwa kipengele muhimu katika kuendeleza ukuaji wa uchumi."

Katika hatua nyingine, Waziri Dkt.Nchemba ameitaka CISNA kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu kwa mujibu wa sheria za nchi wanachama wa SADC.

Aidha, Waziri Dkt.Nchemba amesema, CISNA inatakiwa kuunga mkono juhudi za kuimarisha mazingira ya usimamizi wa biashara miongoni mwa nchi wanachama, na kubadilishana taarifa ili kuzuia uhalifu.

Vilevile, kusimamia maslahi ya wadau, na kuimarisha usalama wa mifumo ya kifedha katika eneo la SADC.
"Ninafurahi kuona kuwa miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa yakifanywa na CISNA kwa siku za hivi karibuni ni pamoja na kuweka sheria za mfano ambazo zitatumika katika eneo hili ambazo zimeidhinishwa na Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Uchumi la SADC.

"Naomba niwasihi wanachama wa CISNA kuhakikisha kuwa yaliyomo katika sheria hizo za mfano yanaingizwa ipasavyo katika sheria zetu za ndani."

Waziri Dkt.Nchemba amesema,kama ilivyo katika maeneo mengine ya dunia, Kanda ya SADC imekumbana na madhara hasi yanayotokana na janga la UVIKO-19.
Mambo mengine ni mivutano ya kikanda iliyotokana na mzozo kati ya Urusi na Ukraine, migogoro ya Mashariki ya Kati na sasa ukame mkali katika nchi za Kusini mwa Afrika.

"Serikali zetu zinahitaji kuimarisha hatua za kupunguza athari kama hizi na kujenga ustahimilivu wa chumi zetu.

"Pamoja na misukusuko hiyo, mwenendo wa kiuchumi wa nchi nyingi za SADC unaonyesha mwelekeo chanya."

Amesema,Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linatabiri mwelekeo chanya wa ukuaji wa uchumi wa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara ukiwa na ongezeko la wastani wa ukuaji wa pato la taifa.
Ni kutoka asilimia 3.4 mwaka 2023 hadi asilimia 3.8 mwaka 2024, huku nchi nyingi zikitarajiwa kuwa na ukuaji zaidi ya wastani.

Aidha, viwango vya mfumuko wa bei na deni la taifa vinaonyesha utulivu na ukuaji wa kiuchumi.

"Ili kudumisha mwenendo thabiti na chanya wa kiuchumi katika ukanda huu, kunahitajika juhudi za pamoja kutoka kwa wadau wote.
"Baadhi ya hatua muhimu katika kuharakisha ukuaji wa kiuchumi wa kanda yetu ni pamoja na kutekeleza mikakati ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Kuendeleza utekelezaji wa malengo ya huduma jumuishi za kifedha na kusaidia maendeleo ya biashara changa na za kibunifu."

Pia amesema, ushirikiano unahitajika katika kukabiliana na vitisho vya uhalifu wa kifedha vinavyoweza kutokea ikiwemo utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi. 

"Ninafurahi kutambua kuwa juhudi hizi ni miongoni mwa vipaumbele katika ajenda za kimkakati za CISNA."

Gavana Tutuba

Awali, Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema kuwa,CISNA ilianzishwa chini ya Kurugenzi ya Fedha, Uwekezaji na Forodha ya Sekretarieti ya SADC.

Amesema,kamati hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kubadilishana kwa taarifa na uzoefu miongoni mwa mamlaka kuhusu masuala ya udhibiti na usimamizi wa masuala ya bima, masoko ya mitaji, pensheni na huduma za fedha zisizo za kibenki.

"Jukumu kuu la CISNA ni kuoanisha kanuni na miundo ya usimamizi ya nchi wanachama na kuhakikisha kuwa zinakidhi viwango vya kimataifa vilivyowekwa na taasisi za viwango za kimataifa.

"Kwa muktadha huo, Benki Kuu ya Tanzania iliona umuhimu wa kujiunga na Kamati hii.
"Hivyo, mnamo Oktoba 2023, katika Mkutano wa 46 wa CISNA uliofanyika Swakopmund, nchini Namibia, Benki Kuu ilijiunga rasmi na CISNA.

"Kwa niaba ya taasisi zinazosimamia sekta ndogo za masoko ya mitaji, bima na huduma ndogo za fedha nchini Tanzania ambazo ni Benki Kuu ya Tanzania (BOT),

"Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) napenda kuwakaribisha wageni wote kwenye mkutano huu."

Gavana Tutuba amaesema, anatarajia mkutano huu wa CISNA hapa Zanzibar utaacha kumbukumbu nzuri na ambayo itakudumu vichwani mwa washiriki kwa muda mrefu."

Mwenyekiti CISNA

Mwenyekiti wa Kamati ya Mamlaka za Usimamizi wa Bima, Masoko ya Mitaji na Huduma za Fedha zisizo za Kibenki (CISNA),Bw. Kenneth Matomola amesema,CISNA ilianzishwa kutokana na azma ya kikanda ya kuunganisha kanuni na mifumo ya uendeshaji ya nchi wanachama wa SADC.
Amesema,lengo ni kuhakikisha kuwa mifumo hiyo inakidhi viwango vilivyowekwa na mashirika ya kimataifa.

Matomola amesema,kamati hiyo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na utaalamu pamoja na kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa sekta ndogo za bima, masoko ya mitaji na huduma za fedha zisizo za benki.

Amesema, mkutano huo wa 47 wa Mwaka wa Kamati ya Mamlaka za Usimamizi wa Bima,Masoko ya Fedha na Taasisi za Fedha zisizo za Kibenki (CISNA) chini ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ulianza Septemba 29 na utafikia tamati Oktoba 4,2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news