Waziri Kombo ahimiza ushirikiano na nchi marafiki ujikite katika biashara

HELISINKI-Tanzania imesisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na nchi marafiki, ikiamini kuwa hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi. Kauli hiyo imetolewa Oktoba 09, 2024 jijini Helsinki, Finland na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo wakati anashiriki kikao cha Mashauriano ya Kisiasa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Elina Valtonen na Naibu Mawaziri wa Wizara hiyo, Mhe. Pasi Hellman anayeshughulikia masuala ya Maendeleo ya Kimataifa na Mhe. Jarno Syrjälä anayeshughulikia Biashara za Kimataifa.
Waziri Kombo amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mabadiliko makubwa ya mifumo ya sera na sheria ili kuboresha mazingira ya biashara kwa lengo la kuvutia uwekezaji nchini Tanzania.

Hivyo, ametoa wito kwa wawekezaji wenye mitaji na dhamira ya dhati ya kuwekeza, waondoe hofu kuhusu Tanzania, kwani nchi hiyo ni mahali salama kwa wawekezaji na mitaji yao.

Waziri Kombo ameishukuru Serikali ya Finland kwa kufanya juhudi kubwa ya kuisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali kama vile misitu, TEHAMA, mifumo ya ulipaji kodi, hali ya hewa na elimu.

Alisema juhudi hizo zimechangia kuifikisha Tanzania hapa ilipo na kuwaomba mawaziri hao waendeleze juhudi hizo, huku wakihimiza kampuni za nchi yao kuja kuwekeza Tanzania ambayo ina fursa nyingi hazijaweza kutumiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mitaji midogo na teknolojia duni.

Maeneo ambayo Balozi Kombo ameyainisha kwa Finland kuyapa kipaumbele katika ushirikiano wake na Tanzania ni pamoja na uhawilishaji wa teknolojia (technology transfer), nishati, viwanda vya kuongoza thamani, elimu ya ufundi, masuala ya kijinsia na haki za wanawake na masuala ya kidijiti.

Amesema maeneo hayo yakifanyiwa kazi ipasavyo, yataongeza nafasi za kazi na ni suluhisho la moja kwa moja la tatizo la ajira nchini.
Mhe. Kombo aliendelea kwa kusema kuwa ni wakati muafaka wa nchi ya Finland kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana wa Tanzania katika fani ambazo nchi hiyo pia inazihitaji kwa kiasi kikubwa.

Amesema Tanzania ipo tayari kutuma vijana ambao watasomeshwa kwa viwango vinavyohitajika katika fani hizo ili kuziba pengo kama vile la wataalamu wa afya hasa manesi katika nchi za ulaya.

Viongozi hao pia walijadili suala la amani na usalama duniani na kusisitiza umuhimu wa kutatua migogoro inayoendelea kwa njia za kidiplomasia.

Waziri Kombo aliwahakikishia viongozi hao kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika suala la kulinda amani na kwamba hivi sasa, Rais Samia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mhe. Waziri alisema kuna sababu mbalimbali zinazosababisha migogoro barani Afrika ikiwa ni pamoja na uwepo wa vijana wengi wasio kuwa na ajira.

Alisema nchi zilizoendelea hazina budi kusaidia programu za kuongeza ajira kwa vijana ambao idadi yao ni zaidi ya asilimia 70 barani Afrika.
“Tusaidiane kutatua changamoto za vijana barani Afrika kwa kuwa migogoro itakayosababishwa na vijana, nchi zitakazoathirika na migogoro hiyo sio Afrika pekee, bali hata Ulaya itaathirika kama inavyotokea katika baadhi ya nchi za Kaskazini mwa Afrika,”Waziri Kombo alisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news