*Aagiza kusimamishwa kazi kwa Bi. Annie Maugo wa Kitengo Jumuifu cha Amana, TAMISEMI
*Aipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kwa kuchukua hatua za awali
DAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameelekeza kufikishwa mahakamani mara moja kwa maafisa wanne wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na watumishi wanne wa kitengo cha Akaunti Jumuifu ya Amana (TSA) kilichopo TAMISEMI kwa tuhuma za ubadhirifu wa shilingi milioni 165.6.
Aidha,ameagiza Bi. Annie Nyabugumba Maugo wa Kitengo cha Akaunti Jumuifu ya Amana asimamishwe kazi kutokana na ushiriki wake kwenye muamala uliohamisha fedha kutoka TAMISEMI kwenda katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.
Ametoa maagizo hayo leo Jumapili, Oktoba 06, 2024 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi. Waziri Mkuu yupo mkoani Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Mheshimiwa Majaliwa amefikia maamuzi hayo kutokana na uchunguzi uliofanywa na timu aliyoiunda kufuatilia tuhuma za ubadhirifu huo pamoja na ukaguzi maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ili kujiridhisha na ukweli wa tuhuma hizo.
Waziri Mkuu amesema kuwa matokeo ya timu ya uchunguzi aliyoiunda yalionesha kuwa watumishi hao walikuwa wanatumia akaunti ya Amana kuficha fedha hizo tofauti na malengo ya matumizi ya akaunti hiyo.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Septemba 05, 2022 watumishi watatu wasio waaminifu kutoka TAMISEMI walishirikiana na watumishi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kuleta shilingi milioni 165.6 na kuzihifadhi kwenye akaunti ya Amana na zikakaa mwaka mzima bila Mkurugenzi, Baraza la Madiwani na Wakuu wa Idara wengine kujua.“Watu hawa wachache walikutana Dodoma, wakati wa mapitio ya mahitaji ya fedha kwa ajili ya Halmashauri na wakakubaliana na maafisa wa kitengo cha fedha za Halmashauri wa TAMISEMI, Bw. Aidan Mponzi, Adora Mwombeki Mbalilaki na kukubaliana wataingiza fedha lakini baada ya muda fedha hizo wazirudishe na fedha zikaingia na baada ya muda wakaanza kufanya matumizi.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa walianza kutumia fedha hizo bila kulijulisha Baraza la Madiwani na bila kuingizwa kwenye bajeti ya Halmashauri ili wakuu wengine wa idara wajue kwamba kuna fedha.
Ameongeza kuwa baada mtandao huo kujulikana, timu ya uchunguzi ilifika katika Halmashauri hiyo na kumhoji Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Erasto Kiwale ambaye alikiri kutofahamu kuhusu uwepo fedha hizo.
“Mkurugenzi alimuuliza Mkuu wa Kitengo cha Fedha cha Halmashauri, Bw. Geofrey James Martin ambaye alikiri kuwepo kwa fedha hizo na Mkurugenzi alimtaka kuzirejesha zilipotoka kwa kuwa hazikuwa na maelezo ila Bw. Geofrey Martin hakufanya hivyo na alipokuja kuhojiwa na timu ni kwa nini hakuzirejesha alisema fedha hizo zimetumwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya MDH (Management and Development for Health) lakini hata Mganga Mkuu wa Wilaya hafahamu kama ameletewa fedha.”
Ameongeza kuwa Bw. Geofrey alipohojiwa zaidi alikuwa muwazi na kukiri kwamba fedha hizo zimeletwa na watumishi wa TAMISEMI kwa makubaliano kuwa sehemu ya fedha hizo zikishatumwa zirejeshwe kwa Bw. Idan Zabron.
Alieleza kuwa,fedha hizo hazijatambulishwa kwa Baraza la Madiwani kwa kuwa zilitumwa kinyume na taratibu.
Amesema kuwa, fedha hizo zilianza kufanyiwa matumizi ambapo milioni 105.6 zikalipwa kwenye maboresho ya barabara inayoelekea dampo la Lingate.
“Fedha hizi zililipwa mara tatu, ambapo shilingi milioni 77.5 alilipwa mzabuni anayeitwa Konya Investiment Company Ltd, shilingi milioni 28.1 zililipwa kwa mzabuni anaitwa Mbogolo Investiment Company na shilingi milioni 2.4 ilikuwa ni posho ya msimamizi.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa timu ya uchunguzi ilipotembelea eneo la mradi na kumhoji mkuu wa mradi, Bw. Godwin Adamson Cheyo ambaye alisema ujenzi wa barabara hiyo ulikuwa ni wa udongo badala ya changarawe na gharama zote za mradi hazikuzidi milioni 30.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa,timu ya uchunguzi ilibaini barabara ilijengwa kwa Udongo badala ya changarawe na gharama zote za mradi hazikuzidi milioni 30.
Pia wazabuni waliotekeleza Mradi hawakuwa na sifa na walitumika tu kupishia fedha, na Bw. Jonathan Stanley Manguli ambaye ni mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ni mtia saini wa kampuni ya Mbogolo Investiment Company na wanatumia anuani moja na Konya Investiment Company Ltd” hivyo kuwepo na mgongano wa kimaslahi.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kwa kuwasimamisha kazi watumishi waliohusika na tuhuma hizo na wengine kufukuzwa kazi.
“Niwapongeze sana kwa kuchukua hatua, na hasa Mkurugenzi unapokuja kupewa taarifa na ukajiridhisha kuwa fedha hizi siyo stahili yetu ulishawaambia wazirudishe wao kwa kuwa walikuwa na mchezo wao, hawakuzirudisha.”