Waziri Mkuu anatarajiwa kuzindua Wiki ya Vijana Oktoba 11-Waziri Ridhiwani Kikwete

DODOMA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Ridhiwani Kikwete amesema zaidi ya vijana 1,000 wanatarajiwa kushiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa mkoani Mwanza yatakayozinduliwa Oktoba 11, 2024.
Aidha, Waziri Ridhiwani Kikwete amesema Wiki hiyo huadhimishwa kila Mwaka Oktoba 8 hadi 14 kwa kuwakutanisha vijana kutoka Tanzania Bara na Visiwani kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kujadiliana, kuonesha vipaji, bunifu na kazi wanazozifanya.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mhe. Ridhiwani amesema, Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua wiki hiyo katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.

Waziri Ridhiwani ametaja shughuli zitakazofanyika kwenye wiki hiyo kuwa ni pamoja na kuwapo na makongamano ya kuwajengea uelewa wa fursa za ujasiriamali, ubunifu wa kidijitali katika kujifunza na kujiajiri sambamba na elimu ya Sera mpya ya maendeleo ya vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024.

Pia, amesema kutakuwa na maandamano ya amani ambayo vijana watabeba jumbe mbalimbali ambazo serikali itazifanyia kazi.

“Kutakuwa na maonesho ambayo hutoa fursa kwa vijana kuonesha bunifu zao na kwa wadau wa maendeleo ya vijana kutoa huduma, elimu na taarifa kwa jamii hususan zile zinazoendana na malengo ya Taasisi zao na zenye lengo la kuleta mabadiliko chanya na kuhamasisha ustawi na maendeleo ya vijana nchini,” amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news