MBEYA-Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa jitihada zake za kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala muhimu ya fedha, hususan utoaji wa leseni kwa taasisi ndogondogo za fedha, fursa za uwekezaji, na ununuzi wa dhahabu kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu nchini.
Prof. Mkenda ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la Benki Kuu wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika katika uwanja wa Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.
Kaimu Mkurugenzi wa Tawi la BoT Mbeya, Bi. Graceana Bemeye, akimkaribisha Waziri Mkenda kwenye banda hilo, alibainisha kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi wanaotembelea banda la Benki Kuu.
Bi. Bemeye alisema kuwa wengi wamekua na shauku ya kujua jinsi Benki Kuu inavyopambana na ongezeko la taasisi zinazotoa mikopo bila leseni, kupitia mitandao na hata mitaani.
Mikopo hiyo isiyo rasmi, inayojulikana kama "mikopo kausha damu," imekuwa ikiathiri wananchi kwa kiwango kikubwa.
Alieleza kwamba Benki Kuu inaendelea na jitihada za kutoa elimu ili kukabiliana na tatizo hilo katika jamii.
Aidha, Bi. Bemeye alisisitiza kuwa Benki Kuu itaendelea kuelimisha wananchi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuhusu umuhimu wa elimu ya fedha, ambayo ni msingi wa maendeleo ya uchumi wa nchi.