ARUSHA-Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ameutaka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuendeleza ushirikiano na Mahakama ili kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.
Mhe. Ridhiwani amesema hayo Septemba 7, 2024 jijini Arusha wakati akifunga Kikao Kazi kati ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania na Menejiment ya WCF.
"Ushirikiano wa mahakama na WCF unadhihirisha umuhimu katika kuwahudumia watanzania kwa kuhakikisha sheria za kazi hususan sheria ya fidia inatekelezwa kwa ufanisi" amesema.
Aidha, Mhe. Ridhiwani amesema Serikali imeongeza kiwango cha chini cha mshahara kinachotumika kukokotoa fidia kwa mwezi ikiwa ni uwezeshaji mkubwa wa kipato kwa watumishi wenye viwango vidogo vya mshahara.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji wa WCF, Mahakama ya Rufaa Tanzania, Kamishna wa Kazi, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Watendaji kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.