DAR-Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ameipongeza Shule ya Sekondari Kinyerezi ya jijini Dar es Salaam kwa kuwalea wanafunzi kwa mrengo wa kisasa hali inayopelekea kuibua na kukuza vipaji vingi miongoni mwa wanafunzi hao huku akiwataka wanafunzi hao kuwa na nidhamu ili kunufaika na vipaji vyao.
Amesema,katika dunia ya sasa kwenye sanaa ndiko kuna uwanja mkubwa wa ajira Mhe.Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Oktoba 12, 2024 wakati akizungumza kwenye mahafali ya 15 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kinyerezi iliyopo katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salam.
"Nimefarijika kuona vipaji vya kila aina, nimewaona wasanii wenye vipaji vikubwa na pia nimeambiwa kuna mwanafunzi kwa sasa yupo Uingereza alichukuliwa tu mara baada ya kuhitimu masomo yake kutokana kipaji kikubwa alichonacho cha kucheza mpira," amesema Mhe.Simbachawene.
Amesema, makuzi ya mrengo wa kisasa kwa wanafunzi wa sasa ni jambo lisiloepukika kwa vile wanafunzi walio wengi wanaohitimu masomo yao hawarudi vijijini kulima.
Kufuatia hatua hiyo Mhe.Simbachawene amewataka wahitimu hao wa kidato cha nne na wanafunzi wanaoendelea na shule licha ya vipaji walivyonavyo wajitahidi kusoma kwa bidii huku akiwasisitiza kujiepusha kuiga tamaduni za kigeni ambazo haziendani na tamaduni zetu.
Katika hatua nyingine, Mhe.Simbachawene amempongeza Rais Mhe.Samia Suluhu Hasssan kwa kukubali kutoa kiasi cha Sh. Bilioni 28 kwa ajili ya jiji la Dar es Salaam ili ziweze kutumika kwenye ujenzi wa madarasa.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu kwenye mazingira bora na ya kisasa ili kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma katika kutimiza ndoto zake.