Waziri Simbachawene asisitiza utekelezaji wa miradi kwa usahihi

NA VERONICA MWAFISI
Serengeti

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka viongozi wa Mkoa wa Mara kutekeleza miradi ya maendeleo kwa usahihi ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kutumika kikamilifu na wananchi.
Akizindua mradi wa Zahanati ya Getarungu uliofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani kupitia Shirika ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) tarehe 3 Oktoba, 2024 wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, amesema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa zahanati hiyo na kutaka halmashauri za mkoa huo kuiga utekelezaji wa namna hiyo.
“Nimefurahi sana, kupitia ziara hii nzuri, kubwa nililojifunza ni utekelezaji wa miradi kwa usahihi sana, tujifunze na sisi halmashauri kuangalia miradi inayotekelezwa kwa usimamizi mzuri inavyokuwa na je sisi tunashindwa wapi? Mhe. Simbachawene amehoji.

Amesema,mradi huo wa zahanani ya Getarungu umesimamiwa na Mkandarasi Maalum na umekuwa ni wa kuridhisha sana, lakini kwenye halmashauri ambako Wakandarasi wanalipwa mishahara, miradi yao inakuwa sio ya kuridhisha.

“Nimezindua zahanati hii ya Getarungu kwa kujidai sana, ni nzuri inafurahisha, nawasisitiza viongozi katika halmashauri kuiga mfano huu mzuri, tukiendelea kutosimamia kwa usahihi tutachukuliana hatua," Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Amesema, utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya jitihada za kukuza sekta ya utalii, kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya utalii na kujenga mahusiano mazuri na wadau wa maendeleo na ndio sababu ya kupatikana kwa mradi huu wa zahanati 8 kwa mara moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ikiwemo hiyo aliyoizindua leo ya Getarungu.
Mhe. Simbachawene ameendelea na ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika Mkoa wa Mara, ambapo leo ametembelea Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Butiama na kuzindua miradi mbalimbali ikiwemo zahanati ya Getarungu, barabara ya kituo kipya cha mabasi Koreri na Shule ya Msingi Chief Manyori.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news