Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana ateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Commonwealth

APIA-Mkutano wa 27 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika Apia, nchini Samoa umemteua Mheshimiwa Shirley Ayorkor Botchwey, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ujumuishwaji wa Kanda wa Ghana kuwa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth).
Katika mkutano huo uliofanyika kuanzia Oktoba 21 hadi 26, 2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Mahmoud Thabit Kombo.

Mbali na kumchagua, Mheshimiwa Botchwey katika mkutano huo masuala mengine nyeti yaliyojadiliwa ni pamoja na uwekezaji, kutafuta suluhu ya pamoja kwa ajili ya maendeleo endelevu, mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia, uchumi, demokrasia, na amani.

Aidha, kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni Ustahimilivu katika Kufikia Malengo ya Pamoja ya Kimaendeleo (One Resilient Common Future: Transforming Our Common Wealth).

Commonwealth ni jumuiya ya hiari inayoundwa na mataifa 56 huru na sawa huku ikikadiriwa kuwa na wanachama zaidi ya bilioni 2.7, ambapo zaidi ya asilimia 60 ni watu wenye umri wa miaka 29 au chini.

Jumuiya hiyo inatajwa kuendelea kupanuka mwaka hadi mwaka duniani kote na inajumuisha mataifa mbalimbali yenye uchumi wa kati, wa juu na yanayoendelea kiuchumi.

Aidha,nchi 33 kati ya wanachama wa Commonwealth ni nchi ndogo, nyingi ikiwa ni mataifa ya visiwa.

Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola inasaidia nchi wanachama kujenga taasisi za kidemokrasia na ujumuishi, kuimarisha utawala na kukuza haki na usawa binadamu.

Vilevile,kazi ya jumuiya hiyo ni kusaidia kukuza uchumi na kuongeza biashara, kuimarisha ustahimilivu wa kitaifa, kuwainua vijana, na kushughulikia vitisho kama vile mabadiliko ya tabianchi, madeni na usawa.

Nchi wanachama zinapata msaada kutoka kwa mtandao wa zaidi ya mashirika 80 ya Serikali, jamii za kiraia, kitamaduni na kitaaluma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news