Wizara ya Ardhi yaja na Mpango wa Uendelezaji eneo la Sinza jijini Dar es Salaam

NA MUNIR SHEMWETA
WANMM

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inakuja na mpango wa uendelezaji upya eneo la Sinza jijini Dar es Salaam (Sinza Redevelopment Plan 2024-2044).
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akisisitiza jambo wakati wizara yake ikiwasilisha taarifa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii tarehe 17 Oktoba 2024 jijini Dodoma.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 17 Oktoba 2024 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakati wa uwasilishaji taarifa ya mradi wa Kupanga, kupima na kumilikisha Ardhi (KKK).

Akiwasilisha taarifa ya mradi huo mbele ya kamati hiyo, Mratibu wa mradi wa KKK Bw. Godfrey Machabe amesema, wizara inaandaa mpango wa uendelezaji upya wa maeneo kongwe katika Mkoa wa Dar es Salaam

"Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa Ubungo pamoja na wadau wengine imeandaa Mpango wa Uendelezaji Upya eneo la Sinza (Sinza Redevelopment Plan 2024 - 2044)," amesema Machabe.
Kamishna wa Ardhi Nchini Nathaniel Methew Nhonge akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Malisili na Utalii tarehe 17 Oktoba 2024 jijini Dodoma.

Amebainisha kuwa, mpango wa uendelezaji upya katika eneo hilo ni mkakati wa kina kwa ajili ya kufufua maeneo ambayo yamezorota na kupoteza thamani pamoja na uhalisia.

Kwa mujibu wa Mratibu huyo wa Mradi wa KKK, mpango huo unatekelezwa eneo la Sinza kutokana na sababu mbalimbali kama vile ukuaji wa kasi na majengo marefu, ongezeko kubwa la watu na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii pamoja na ongezeko la uhitaji wa huduma za kijamii na miundombinu kutokana na ongezeko la watu.

Mpango huo umepanga kujumuisha mabadiliko ya matumizi ya ardhi, kujenga na kuboresha miundombinu pamoja na kuboresha huduma za jamii na miundombinu ya huduma za jamii kama vile Usafiri, maji safi, maji taka, maji taka, maji ya mvua, umeme, taka ngumu, mifumo ya gesi, nishati ya umeme na mawasiliano.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Malisili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava akizungumza wakati Kamati yake ikipokea na kujadili taarifa za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi tarehe 17 Oktoba 2024 jijini Dodoma.

Kwa upande wake, Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii chini ya mwenyekiti wake Mhe. Timotheo Mzava imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi unaotekelezwa na wizara ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

"Tumeridhishwa na utekelezaji mradi wa KKK ukiwemo huu mpango wa kuendeleza maeneo kongwe ikiwemo eneo la Sinza,"amesema Mhe. Mzava.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhe. Geophrey Pinda amesema, wizara yake inafuatilia maeneo ya miji mikongwe kwa lengo la kuona namna ya kuyaboresha ili kuendana na kasi ya ukuaji wa maendeleo.

Akigeukia mradi wa KKK katika Mwaka 2023/24, Naibu Waziri wa Ardhi amesema Wizara yake ilihuisha akaunti ya Mfuko wa Maendeleo ya Ardhi (PDRF) kwa ajili ya utekelezaji miradi ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi, mfuko alioueleza kuwa utakuwa ukitoa fedha kwa Halmashauri kutekeleza miradi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Upendo Matotola akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kuhusu hatua iliyofikia kwenye uanzishwaji wa Mamlaka ya Sekta ya Milki nchini tarehe 17 Oktoba 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

Kwa mujibu wa Mhe. Pinda, Mfuko huo umeandaliwa Mwongozo wa uratibu na utekelezaji kwa ajili ya kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imepokea na kujadili taarifa za wizara ya ardhi zinazohusu Utekelezaji Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK), Hatua iliyofikiwa katika Uandaaji wa Sera ya Ardhi pamoja na taarifa ya hatua iliyofikiwa kwenye Uanzishwaji wa Mamlaka ya Sekta ya Milki nchini (Real Estate Authority).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news