Wizara ya Madini na Barrick zaanza mikakati ya kuwaandalia mazingira rafiki wachimbaji wadogo

KAHAMA-Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Kampuni ya Dhahabu ya Barrick zinatarajia kuanza mikakati ya kufanya utafiti katika maeneo yenye leseni mkoani Mara yatakayotumiwa na wachimbaji wadogo wa madini baada ya utafiti kukamilika ikiwa ni lengo la kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo ili wachimbe kwa tija.
Hayo yamesemwa Oktoba 5,2024 na Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Mkutano wa Uwasilishaji wa Taarifa ya Utekelezaji ya Robo Mwaka ya kampuni ya Barrick mkoani Shinyanga.

Dkt.Kiruswa amesema kuwa, kwa kipindi kirefu Mgodi wa North Mara umekuwa na changamoto ya kuvamiwa na wachimbaji wadogo unaoambatana na uharibifu wa mali ambapo kupitia majadiliano ya pamoja tumekubaliana kuunda timu itakayofanya tafiti katika leseni 13 na baadae kuyakabidhi kwa wachimbaji wadogo kwa utaratibu maalum utakaojumuisha ngazi mbalimbali za kiutendaji.
Dkt.Kiruswa amesema, Kampuni ya Barrick imekuwa na mchango mkubwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa migodi yote kuendelea ili shughuli za uchimbaji zifanyike kwa usalama pamoja na wachimbaji wadogo kupata maeneo mazuri ya uchimbaji.

Akielezea kuhusu timu ya utafiti Dkt.Kiruswa ameeleza kuwa, makubaliano ya awali ni kuunda timu itakayojumuhisha wataalam kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini, Kampuni ya Barrick, Uongozi wa Mkoa , wawakilishi wa wachimbaji wadogo ambapo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Oktoba 15, 2024 jijini Dodoma.
Kwa upande wake, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick , Mark Bristow amesema kuwa utafutaji wa madini unaoendelea katika maeneo yaliyotumika na kuachwa kwenye migodi ya Bulyanhulu na North Mara unaendelea ambapo tayari maendeleo mazuri yanayoweza kuongeza migodi mipya kwa Barrick.

Akielezea kuhusu michango ya Barrick kwa jamii Bristow amesema , kupitia mpango wa Bartick na Twiga wa kusongesha mbele Sekta ya Elimu tayari mpaka sasa ujenzi wa shule zipatazo 64 zikiwa na thamani ya dola milioni 10, ikiwa pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa 396, mabweni 97 yamejengwa.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Msalala Iddi Kassim Iddi amezipongeza kampuni ya Twiga na Barrick kwa juhudi za maendeleo kwa jamii inazofanya kupitia Mpango wa Ushirikishwaji wa jamii inayozunguka mgodi hususani katika Sekta ya Elimu , Miundombinu ya Barabara na Ujenzi wa Vituo vya Afya.
Sambamba na hapo, katika kutambua juhudi zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali kampuni za Twiga na Barrick zimetoa kiasi dola za Marekani elfu 30 kwa asasi na mashirika ya kijamii.

Mkutano huo umejumuisha viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya mkoa , wilaya , kata na vitongoji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news