NA SAMUEL MTUWA
IMEELEZWA kwamba katika kuendeleza shughuli za uchimbaji mdogo wa madini nchini na kuhakikisha rasilimali madini zinaongoza kuchangia katika Pato la Taifa , wizara na taasisi zake zinaendelea kutekeleza mikakati na mipango kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Akielezea kuhusu mikakati iliyopo ndani ya wizara kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025, Waziri Mavunde amesema kuwa, katika kuimarisha uchimbaji wenye tija na uhakika serikali itajenga maabara ya kisasa mkoani Dodoma na Geita ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupeleka sampuli zao kwa uchunguzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa madini Dkt. Steven Kiruswa ameeleza kuwa, elimu kuhusu tozo zinazotozwa, wajibu wa mmiliki wa leseni kwa jamii, ushiriki wa watanzania katika uvunaji wa rasilimali madini na utunzaji mazingira katika shughuli za uchimbaji ilitolewa kwa wachimbaji wadogo katika Kamati za Maendeleo za Kata.
Awali, akiwalisha taarifa kuhusu mikakati ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwasogezea huduma za Ugani katika mkoa wa Dodoma kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulhRaman Mwanga amesema, wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya zebaki katika wilaya ya Chamwino na Bahi.

Mikakati mingine ni pamoja na kutoa elimu kuhusu athari za mazingira zitokanazo na uchimbaji wa madini ujenzi, elimu kuhusu tozo za madini na haki madini katika wilayani ya Dodoma na vitongoji vyake.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati wa Kamati ya Bunge Nishati na Madini Dkt.David Mathayo David, ameipongeza wizara kwa juhudi mbalimbali inazofanya katika mnyororo mzima wa thamani madini kutoka asilimia 7.1 mpaka kufikia asilimia 9 katika kuchangia Pato la Taifa.
