Wizara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar yaja na Kampeni ya Kitaifa ya Mtoto Mboni Yangu

ZANZIBAR-Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Taasisi ya Ndoto Ajira kutoka Dar es Salaam imeandaa kampeni ya kitaifa yenye jina la Mtoto Mboni Yangu ambayo itafanyika katika mikoa mitano ya Zanzibar.
Hayo yamesemwa Oktoba 25,2024 jijini Zanzibar na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mheshimiwa Riziki Pembe Juma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kampeni ya Kitaifa ya Mtoto Mboni Yangu.

"Lengo kuu la kampeni hii ni kukusanya fedha kwa ajili ya kuizunguka nchi nzima na kuielimisha, kuiasa na kuzungumza na Wazanzibari wote wakiwemo wanafunzi, viongozi wa dini, vijana, watoto na jamii kwa ujumla juu ya kupinga vitendo vyote vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto, vijana, wanawake na wazee.

"Ili kwa pamoja tuweze kuwalinda watoto na vijana wetu dhidi ya mmongonyoko wa maadili."

Waziri Pembe amesema,Kampeni ya Mtoto Mboni Yangu imeanza Oktoba 23 na itaendelea hadi Disemba 30, 2024 ikiwa ni kampeni ya miezi miwili.

Aidha, amesema kampeni ya MTOTO MBONI YANGU itazinduliwa pia kwa mbio za Marathon siku ya Jumamosi ya tarehe 23 Novemba 2024 katika viwanja vya Mao Tse Tung.

"Na kufungwa katika visiwa vya Pemba. Ni imani yangu kwamba jamii itaunga mkono juhudi hizi.

"Kampeni hii imekuja ikiwa na azma ya kuunga mkono juhudi za mhe Rais wetu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Serikali ya Awamu ya Nane ambapo tunaziona juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali yetu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu na kupambana na vitendo vyote viovu vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia."
Waziri Pembe amesema,kupitia kampeni hiyo, Wizara inategemea kukusanya kiasi cha shilingi milioni 650 ambazo zitatumika katika utekelezaji wa kampeni hiyo.

"Hivyo, tunaiomba jamii, kuitikia wito huu kwa kuchangia fedha ili zoezi hili liweze kufanikiwa kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

"Marathon yetu inatarajiwa kujumuisha takriban washiriki 20,000, kutoka Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara wakiwemo watoto, vijana, wanawake, watu wazima kwa jinsia zote na hali zote bila kumuacha mtu nyuma (wakiwemo na watu wenye ulemavu).

"Washiriki wote wa Marathon watapewa medali baada ya kumaliza mbio za kilomita 21 (nusu marathon), kilomita 10, na kilomita 5, huku washindi watano wa mwanzo watapewa zawadi za fedha taslimu."

Waziri Pembe amesema,MTOTO MBONI YANGU MARATHON ni Marathon ya kwanza kufanyika ndani ya Zanzibar.

"Tunaomba wananchi wote na wadau wote kujitokeza kuchangia kampeni hii. Tutoe wito kwenu pia ndugu wana habari kuwa wa kwanza kujitokeza kuchangia kwani shilingi yako moja ndio mwanzo wa hesabu.

"Hii ni nafasi ya kipekee kwa kuunga mkono juhudi za Serikali yetu ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya nane katika kulinda vizazi vyetu viwe vyenye maadili mema kwa maendeleo ya taifa letu.

"Gharama ya kujisajili kwa mtu mmoja mmoja ni shilingi 30,000 ambapo mshiriki atapata Tshirt na namba yake."
Amesema,pia kwa mara ya kwanza wameleta vifurushi kwa makampuni na taasisi mbalimbali wana nafasi ya kuchangamkia vifurushi.

"Package ya milioni 1,000,000 kampuni au taasisi itaweza kupata T-shirt 10 za marathon, logo zao kuonekana kwenye red capert, kukaa sehemu maalumu siku ya marathon pamoja na kutunukiwa cheti maalumu.

"Package ya 500,000 ambapo kampuni au taasisi itaweza kupata T-shirt 5 za marathon, logo zao kuonekana kwenye red capert, kukaa sehemu maalumu siku ya marathon na kutunukiwa cheti maalumu.

"Kwa pamoja tukishirikiana tunaweza kulitokomeza janga hili ndani ya nchi na Taifa letu ili kuwa na kizazi chenye maadili mema, kinacho weza kuchangia mustakabal bora wa taifa letu.Zanzibar bila ya udhalilishaji inawezekana sana endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake,"amesisitiza Waziri Pembe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news