Yanga SC kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto

DAR-Klabu ya mpira ya Yanga imeahidi kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto wasio na uwezo, kutoa uelewa kwa jamii kuhusu magonjwa ya moyo na kutangaza huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
Hayo yamesemwa Oktoba 2,2024 jijini Dar es Salaam na Rais wa klabu ya Yanga Eng. Hersi Said wakati akizungumza na viongozi wa JKCI walipomtembelea ofisini kwake kwaajili ya kuona ni namna gani klabu hiyo itashirikiana na JKCI.

Eng. Hersi alisema katika ushirikiano huo wataanza kwa kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto kwa kushiriki chakula cha jioni chenye lengo la kuchangisha fedha hizo za matibabu kilichoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete tarehe 2 Novemba mwaka huu katika Hoteli ya Johari Rotana iliyopo jijini Dar es Salaam.

“Taasisi hii imekuwa ikitoa huduma kwa jamii tunahitaji kuwa na ushirikiano nayo kwa muda mrefu kwa asilimia 100, sisi tutaanza kwa kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto wasiokuwa na uwezo kwani tuna ndugu zetu ambao ni wagonjwa wa moyo na sisi pia tunaweza kuumwa hivyo basi ni muhimu kuisaidia jamii yenye uhitaji.

“Pia tutatangaza huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa, tutawapeka wachezaji wetu kupima afya za mioyo yao kwani wanawataalamu waliobobea katika matibabu ya moyo pia wanavifaa vya kisasa vya kupima na kutibu moyo,”alisema Eng. Hersi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema asilimia 70 ya gharama za matibabu ya moyo kwa watoto wanaotibiwa katika taasisi hiyo yanalipwa na Serikali na asilimia 30 iliyobaki inalipwa na JKCI pamoja na wadau mbalimbali.

“Katika taasisi yetu kuna watoto 1500 wanasubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo na asilimia kubwa wanatoka katika familia zenye uchumi mdogo hivyo basi ninawaomba wadau mbalimbali waweze kushirikiana nasi katika kuchangia matibabu ya watoto hawa kwani tatizo ni kubwa na tunahitaji kuwasaidia ili wapate huduma.

“Ninaishukuru klabu ya Yanga kwa kukubali kushirikana nasi katika chakula cha jioni kwa kuchangia gharama za matibabu ya watoto kwani kuna watoto ambao wanatakiwa kufanyiwa upasuaji wa haraka hii ni ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa na kuna wengine wanaweza kusubiri baada ya muda fulani ndipo wakafanyiwa,"alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake mjumbe wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Abdulmalick Mollel aliishukuru klabu ya Yanga kwa kuamua kushirikiana na JKCI katika kuchangia matibabu ya watoto wasio na uwezo na kutoa elimu kwa jamii kuhusu magonjwa ya moyo.

“Magonjwa ya moyo ni moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza na yanaweza kuepukika kama wananchi watafuata ushauri wa kitaalamu hii ikiwa ni pamoja na kuwa na uelewa wa jinsi ya kujikinga na magonjwa haya, ninaamini tukishirikiana kwa pamoja watu wengi watakuwa na uelewa wa kutosha wa magonjwa haya na kuepukana nayo,”alisema Mollel.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news