ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Zanzibar inaendelea kuleta mageuzi makubwa ya miundombinu kwa lengo la kuwavutia wawekezaji.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 4, 2024 Ikulu jijini Zanzibar alipokutana na Rais wa Kampuni ya Samsung C& T Corporation, Oh Se-Chul kutoka Korea Kusini na ujumbe wake.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Zanzibar ina fursa nyingi na kuwakaribisha Zanzibar kuwekeza.
Halikadhalika Dkt.Mwinyi ameuelezea ujumbe huo maeneo ya vipaumbele katika uwekezaji hivi sasa kwa Zanzibar ni Utalii, Uchumi wa Buluu, Uvuvi, Usafirishaji na Mafuta na gesi.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza kampuni ya Samsung C&T kwa wazo la kushirikiana na nchi za Afrika hasa za Kusini mwa Jangwa la Sahara katika nyanja mbalimbali za uwekezaji pamoja na kuanzisha ofisi yao Tanzania. Naye, Rais wa Kampuni hiyo, Bw. Oh Se-Chul amemuelezea Rais Dkt. Mwinyi kwamba, Kampuni hiyo katika kutanua wigo wa uwekezaji, kwa sasa imeamua kuja Afrika na Tanzania kuwa kipaumbele kwenye uwekezaji wao pamoja na kufungua ofisi zao hapa nchini.