ZANZIBAR-Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) Mhe. Mama Mariam Mwinyi amesema Zanzibar inaendelea kuchukua juhudi maaluum za kudhibiti maradhi ya kuambukiza yanayowapata kinamama kipindi cha ujauzito.
Amesema, juhudi hizo zinalenga kuhakikisha ustawi wa mama na mtoto na udhibiti wa changamoto wanazokabiliana nazo, ikiwemo Ukimwi, kifua kikuu na utapiamlo.

Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 8, 2024 katika Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi alipofungua kongamano la siku tatu.
Kongamano hilo linajadili masuala ya afya ya mama na mtoto hususani udhibiti wa maradhi TB, HIV na Malaria linalowashirikisha wataalamu wa Afya ya mama na mtoto kutoka Kenya, Nigeria, Tanzania na Skuli ya dawa za Kitropiki ya Uingereza.




Kongamano hilo la siku tatu litahitimishwa kwa kutolewa ripoti ya miaka mitano ya Mradi wa Udhibiti wa Afya ya mama na mtoto na kukinga na maradhi ya TB, Ukimwi na Malaria.