ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema,Zanzibar inahitaji wadau zaidi kuunga mkono juhudi za kuutunza, kuuhifadhi na kuuendeleza Mji Mkongwe wa Zanzibar kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa nchi.Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 2024, Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na ujumbe kutoka Taasisi ya International National Trust Organization ya Uingereza iliyomueleza mafanikio waliyoyapata katika kulifanyia ukarabati jengo la Custom House liliopo Forodhani maarufu jengo la Mizingani. Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema Mji Mkongwe mbali ya kuwa ni eneo la Urithi wa dunia pia ni muhimu la kukuza Uchumi wa Zanzibar kupitia Sekta ya Utalii kwani linalotembelewa na wageni wengi.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kufarajika kwake na juhudi na hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe (JUHIMKO) kwa kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la Mizingani.
Akizungumzia changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kuongezeka na kina cha bahari, Meneja miradi wa Taasisi ya International National Trust Organization, David Antony Simpson amesema, ni miongoni mwa changamoto inayoikabili miji mingi ya urithi duniani iliyoko pembezoni mwa bahari.
Ni kama ilivyo kwa Mji Mkongwe wa Zanzibar, na kuahidi taasisi yake kuendeleza ushirikiano na Zanzibar kuhakikisha Mji Mkongwe kubaki kwenye ramani ya Dunia.
Vilevile ameeleza kuwa, taasisi hiyo ina uzoefu kwa nchi 102 duniani walizozifanyia ukarabati wa miji mikongwe.