Zanzibar na Arusha kushirikiana Maonesho ya Utalii na Uwekezaji ya Oktoba 25 hadi 26,2024

ARUSHA-Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar,Arif Abbas Manji na Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Mhe. Paul Christian Makonda wamekubaliana kushirikiana pamoja katika kuvutia watalii na wawekezaji mbalimbali kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya Utalii mkoani Arusha na Visiwani Zanzibar.

Ni kwa kutumia vyema maonesho ya utalii na uwekezaji yanayotarajiwa kufanyika Zanzibar Oktoba 25 hadi Oktoba 26, mwaka huu.
Ushirikiano huo wa pamoja umefikiwa Oktoba 5, 2024 wakati viongozi wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar walipofika mkoani Arusha kukutana na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Sambamba na viongozi wa waongoza watalii mkoani hapa kama TATO, TLTO na Ngorongoro, lengo likiwa ni kuwaalika rasmi kushiriki kwenye maonesho hayo ya kwanza ya kimataifa yatakayofanyika kwenye kituo cha maonesho Zanzibar-Dimani.

Arusha ni mkoa kinara kwa utalii wa Tanzania Bara, ukitajwa kuiingizia nchi fedha nyingi zaidi za kigeni huku idadi ya watalii ikiongezeka zaidi tangu kuchezwa kwa filamu ya The Royal Tour iliyoongozwa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande mwingine, Zanzibar inasifika kwa utalii wa fukwe barani Afrika, utalii ambao unachangia zaidi ya asilimia 30 kwenye pato la taifa na takribani asilimia 80 ya fedha za kigeni.

TATO na TLTO tayari wamekubali kushiriki kwenye maonesho hayo na kuleta wadau zaidi ya 70 kutoka Arusha.

Ushirikiano huu unalenga kuimarisha sekta ya utalii na kuvutia wawekezaji zaidi, huku maonesho haya yakitarajiwa kuwa jukwaa la kubadilishana maarifa na uzoefu, na hatimaye kukuza utalii endelevu nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news