Zanzibar ni salama kwa utalii wa mikutano na makongamano ya Kimataifa-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar ni nchi salama kwa utalii wa mikutano na makongamano ya kimataifa.Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2024 kwenye Kongamano la Kwanza la Kiislamu la Kimataifa lililowakutanisha Mashehe mbalimbali kutoka mataifa 18 duniani, kwenye viwanja vya "New Amani Complex," Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar ina fursa kubwa ya kukuza utalii wa maadili, "Halal Tourism," kama chanzo cha mapato na ajira kwa watu wake.

Kupitia kongamano hilo la Kiislamu la kimataifa, limetoa mwangaza kwa nchi kama sehemu ya utalii wa maadili, hasa kwa wageni wanaokuja kuitembelea, si tu kujifunza dini lakini pia kufurahia uzuri wa mandhari, haiba ya nchi, mila, silka, utamaduni, na ukarimu wa watu wake.
Halikadhalika, Alhaj Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa mikusanyiko kama hiyo.

Vilevile kuunga mkono jitihada za taasisi binafsi na za serikali, ikiwemo kukuza uchumi na maadili ya nchi ili kupatikane jamii yenye maadili, na kuiweka nchi kwenye hadhi ya utalii wa maadili ambao hivi sasa umeshika kasi duniani.

Naye, Mufti Ismael Menk kutoka nchini Uingereza, ambaye ni mmoja wa watoa mada wakuu katika kongamano hilo amesema, maendeleo ya taifa lolote duniani hayatimii bila kuwepo kwa ustawi wa amani.
Sambamba na usalama kwa nchi na watu wake, kwa kuendeleza na kudumisha umoja, upendo, na kuheshimiana miongoni mwa jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news