Zanzibar yapokea dawa kutoka Global Life Sharing na Taasisi ya Noah

ZANZIBAR-Wizara ya Afya Zanzibar imepokea dawa zenye thamani ya dola za kimarekani milioni moja laki tano sawa na shilingi bilioni 4.2 fedha za Tanzania kutoka Shirika la Global Life Sharing kwa kushirikiana na Taasisi ya Noah ya nchini Korea Kusini.
Msaada huo umehusisha dawa za kutibu magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na dawa za maumivu, pumu, kisukari na magonjwa mengine ambayo yanaendelea kusumbua afya za wananchi.

Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui mara baada ya kupokea msaada huo huko Ofisi za Wakala wa Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi, alisema hatua hiyo ni muendelezo wa mkataba wa mashirikiano baina ya Wizara ya Afya na Taasisi ya Noah juu ya kuwapatia misaada mbalimbali inayoimarisha utendaji kazi wa sekta hiyo.

"Taasisi hizi, mbali na kutupatia misaada ya dawa, lakini imekua ikishirikiana nasi katika mambo mbalimbali ya kuimarisha afya ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo wataalamu wetu wa afya nje ya nchi, kutuunganisha na mashirika ya maendeleo yaliyopo nchini Korea Kusini.

"Mashirika ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya afya hapa nchini pamoja na kuleta wataalamu wao kubadilishana uzoefu na wataalamu wetu katika mambo ya afya,"amesema Waziri Mazrui.

Aidha, aliwaomba wadau na washirika wa maendeleo kuendelea kushirikiana na wizara hiyo katika kutoa misaada mbalimbali itakayoongeza ufanisi wa utendaji katika sekta hiyo na kutoa huduma bora za afya za kwa jamii.

Alisema kuwepo kwa mashirika yanayotoa misaada kama hiyo kutasaidia kufikia malengo ya wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakisha afya za wananachi zinaimarika.

Mazrui ameihakikishia taasisi hiyo kuwa dawa hizo zinafika katika vituo vya afya na hospitali zenye uhitaji ili kumaliza tatizo la kukosekana kwa baadhi ya dawa muhimu zinazohitajiwa na wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar, Abdulhalim Muhammed Mzale alisema, lengo la msaada huo ni kuwafikia wananchi bila malipo yoyote hivyo dawa hizo zitasambazwa katika vituo na hospital kulingana na mahitaji ya maeneo hayo Unguja na Pemba.

Alifahamisha kuwa, dawa hizo ziko salama kwa matumizi ya binadamu kwani taratibu zote za kisheria zilifuatwa wakati wa kuingizwa nchini ikiwemo kukaguliwa na ZFDA.

Aidha alizishukuru taasisi hizo kwa kuwapatiaa msaada huo uliokwenda sambamba na mahitaji ya dawa yaliyopo hivi sasa.

Mkuu wa Taasisi ya Noah, Mama Park na Mwakilishi wa Shirika la Global Life Sharing ya Korea Kusini, Kim walisema kuwa Taasisi hizo zitaendelea kuleta misaada kama hiyo ili kuongeza upatikanaji na vifaa tiba katika hospital na vituo vya afya vilivyo katika maeneo mbalimbali nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news