DAR-Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu 47 kwa kipindi cha Oktoba,2024 kwa tuhuma mbalimbali za kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Hayo yamebainishwa Novemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, SACP Muliro J. Muliro wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema, Oktoba 29, 2024 walikamatwa watuhumiwa 15 kwa tuhuma za wizi wa kontena lililokuwa na vifaa vya kuchimbia madini mali ya kampuni ya Mkuti ambavyo vilikuwa vinasafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya.
Kamanda Muliro amevitaja vifaa hivyo kuwa ni engine machine saba, Digger machine 15, vibuyu vya compresser 90, na Atometer machine mbili.
Amesema,watuhumiwa waliokamatwa siku za nyuma na baadae kufikishwa mahakamani wamepatikana na hatia akiwemo Derick Kiyagoka (32) mkazi wa Kitunda Kati aliyehukumiwa miaka 30 jela na Mahakama ya Kinyerezi kwa kosa la kubaka.
Wengine ni Saidi Kambi (49) mkazi wa Mbagala alifikishwa kwenye Mahakama ya Kinyerezi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kubaka na kulawiti,
Saidi Abdallah alihukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti baada ya kufikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya Kinondoni,
Ayubu Saidi pia alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa unyanganyi wa kutumia silaha, hukumh ilitolewa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.
Mwingine ni Abdala Athumani miaka 31 mkazi Yombo alisomewa hukumu ya kunyongwa hadi kufa na Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni kwa kosa la mauaji,
Iddy Omary Ndekae miaka 26 mkazi wa Mbagala alihukumiwa hukumu ya kunyongwa hadi kufa na Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni kwa kosa la mauaji.
Aidha, ameongeza kuwa jumla ya watuhumiwa 22 walikamatwa kwa kujihusisha na kusafirisha, kuuza na kutumia dawa za kulevya ikiwemo bangi.
Pia wamekamatwa watu 10 kwa tuhuma za kujihusisha na uvunjaji wa nyumba mchana na usiku baadae kuiba.
Mbali na hayo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi lao ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi ili kuziba mianya ambayo wahalifu wanaweza kutumia kutenda uhalifu nchini.