DAR-Chama cha ACT Wazalendo kimezindua rasmi Ilani ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji ya 2024 hadi 2029 huku kikiainisha mambo tisa muhimu kitakachofanya kwa ajili ya kuleta mabadiliko kwa maslahi ya wananchi kama kikipewa ridhaa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo uliofanyika leo Novemba 17, 2024 jijini Dar es Salaam Kiongozi wa chama,Bi. Dorothy Semu ametaja mambo hayo muhimu kuwa ni pamoja na chama na kudhamiria kutoa viongozi waaminifu, jasiri na mahiri katika vijiji, mitaa na vitongoji nchini.
Aidha,mengine ni kudhamiria kurejesha nguvu za serikali za mitaa kwa wananchi na kwamba chama kimedhamiria kuboresha na kuendeleza huduma za jamii kwa wote mijini na vijijini.
Vilevile kimedhamiria kuwahudumia wananchi kwa kutoa huduma bora na stahiki, kusikiliza changamoto zao na kuwa karibu nao.
Bi.Semu ametaja mengine kuwa ni dhamira ya kupambana na rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma, dhamira ya kuimarisha miundombinu vijijini ili kuamsha uchumi, kuzalisha ajira na kuondoa umasikini na dhamira ya kujenga uwezo wa kujitegemea wa serikali za mitaa.
Amesema, wamedhamiria kujenga mitaa na vijiji salama kwa watu kufan ya biashara zao bila bughudha ya migambo, polisi wala sungu sungu pamoja na kudhamiria kutokomeza umasikini vijijini na mijini.
"Ahadi yetu kwenu ni kwamba tutawajibika kwenu, tutatoa huduma bora na kujenga mitaa, vijiji na vitongoji vinavyostawi. Tutajenga mitaa, vijiji na vitongoji vya wote, kwa maslahi ya wote. Tumia nguvu ya kura yako kufanya mabadiliko," amesema Semu.
Hata hivyo, amebainisha kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji wa mwaka huu 2024 unawapa nafasi ya kipekee kufanya mageuzi makubwa katika ngazi hii muhimu ya maamuzi.
Amesema kwamba, uchaguzi huu unawapa nafasi ya kuwa na serikali za mitaa zinazowajibika kwa wananchi, kwa kutoa
huduma bora, kuamsha uchumi na kujenga vijiji, mitaa na vitongoji
vinavyostawi.
"Kupitia uchaguzi huu, tunapaswa turejeshe mamlaka na hatma ya vijiji, mitaa na vitongoji mikononi mwetu."
Amesema, licha ya kutambua umuhimu mahususi wa uchaguzi huu wa serikali za mitaa, maono ya ilani hiyo ni kuhakikisha mageuzi makubwa ya Serikali za mitaa kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, mtaa, kata hadi wilaya.
Bi.Semu amesema kwamba, ilani hiyo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji inawasilisha matumaini, mitazamo na misimamo yetu kwa wananchi.