AFD yaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania utekelezaji wa miradi ya maendeleo

DODOMA-Shirika la la Maendeleo la Ufaransa (AFD) limeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya nishati mabadiliko ya tabia nchi, maji, uchumi wa buluu, kilimo na sekta ya usafirishaji.
Ahadi hiyo imetolewa jijini Dodoma wakati wa Mkutano wa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bw. Jean Francois Arnal, uliojadili kuhusu ushirikiano wa maendeeo kati ya Tanzania na Ufaransa.

Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Mwamba alisema kuwa Ufaransa kupitia Shirika la AFD imeisaidia Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maji, nishati, usafirishaji, kilimo, uvuvi na Uchumi wa buluu, ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo endelevu ya nchi.
Alisema kuwa, mkutano wake na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la AFD, umejadili ushirikiano wa kimaendeleo kati ya pande hizo mbili na kuainisha miradi mipya inayotarajiwa kutekelezwa kupitia Shirika hilo.

Dkt. Mwamba ameishukuru Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la AFD kwa kuendelea kutoa msaada katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoenda sambamba na ajenda ya Taifa ya maendeleo.
Aidha, ameiomba Serikali ya Ufaransa kuendelea kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya kilimo, nishati, maji, miradi ya mazingira, Uchumi wa buluu na usafirishaji ukiwemo mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Dkt. Mwamba, ameiahidi Ufaransa kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo kati ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya wananchi wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bw. Jean Francois Arnal, alisema kuwa Tanzania ni mshirika mkubwa wa Ufaransa kwa upande wa nchi za kusini mwa Afrika, hivyo nchi yake imeongeza ufadhili katika miradi mbalimbali.

Alisema kuwa, Ufaransa inampango wa kuongeza ushirikiano katika miradi ya nishati, mabadiliko ya tabia nchi, maji, uchumi wa buluu, usafirishaji na kilimo.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Mwakilishi Mkazi wa AFD, Bi. Celine Robert, Mtaalamu Mwandamizi wa Masuala ya Miundombinu wa AFD, Bw. Matthieu Bommier, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Robert Mtengule na wajumbe wengine kutoka Wizara ya Fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news