DAR-Shauri la Uhujumu Uchumi Namba 16/2022 limekamilika katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam mbele ya Mhe. Rehema Lyana-Hakimu Mkazi Mkuu kwa Mshtakiwa Bw. Michael Henry Msangawale ambaye alikuwa AFISA TEHAMA wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji Kampasi ya Dar es Salaam kwa kutiwa hatiani baada ya kufanya makubaliano ya maridhiano (plea-bargaining) katika shauri dhidi yake.
Afisa huyo alishtakiwa kwa kosa la kutaka rushwa ya ngono kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 rejeo la mwaka 2019.
Kifungu hicho kinasomwa pamoja na Jedwali la 21 la Aya ya kwanza ya kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Kudhibiti Uhujumu Uchumi (EOCCA).
Mshtakiwa aligoma kumwekea matokeo katika mfumo mwanafunzi mmoja ili aweze kuendelea na masomo yake katika hatua ya Diploma kwa sharti la kupewa ngono.
Mshtakiwa aliomba kufanya majadiliano ya maridhiano wiki iliyopita Mahakama ikaridhia na kumtia hatiani baada ya kukiri kosa na kulipa fidia ya shilingi milioni 10 ambazo atapatiwa mwanafunzi aliyetakiwa kutoa rushwa ya ngono.