Afrika itathmini maliasili zake ili zijumuishwe kwenye GDP-AfDB

DODOMA-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb) ameshiriki kikao kwa njia ya mtandao kujadili Andiko la Kisera kuhusu utajiri wa maliasili, mtaji unaotokana na maliasili na uchumi wenye tija kwa mataifa ya Afrika.
Kikao hicho kilichoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kuhusisha Mawaziri wa Sekta za Mambo ya Nje, Uchumi, Maliasili, Fedha na Mipango kilifanyika Novemba 06, 2024 ambapo Rais wa AfDB, Dkt. Akinwumi Adesina aliwasilisha matokeo ya Andiko hilo kwa Waheshimiwa Mawaziri.
Kwa muhtasari andiko hilo lilibainisha kuwa mataifa ya Afrika yana maliasili nyingi kama misitu na ardhi, lakini nchi hizo hazijaweza kutathimini thamani ya maliasili hizo na kuzijumuisha katika pato ghafi la ndani la nchi hizo yaani Gross Domestic Product (GDP).

Andiko hilo limebainisha faida kubwa za kiuchumi ambazo nchi za Afrika zinaweza kupata endapo zitafanikiwa kutathimini thamani ya maliasili na kuzijumuisha katika GDP.

Faida hizo ni pamoja na kuongezeka thamani ya GDP na kuongezeka kwa hamasa kwa nchi za Afrika kulinda na kutunza maliasili ambazo zina athari chanya katika kudhibiti mabadiliko ya tabianchi duniani.
Akichangia katika kikao hicho kutokea jijini Dodoma, Mhe. Naibu Waziri Chumi alisema Tanzania inaunga mkono Andiko hilo na kutoa wito kwa nchi za Afrika na dunia kwa ujumla kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika agenda yake ya Nishati Salama ya Kupikia.

Alisema agenda hiyo inalenga kulinda mazingira hasa uharibifu wa misitu kwa nchi zinazoendelea.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa Afrika kufanya kazi kwa pamoja, kuwa na taasisi mahsusi za kuratibu tathmini ya maliasili, kutunga Sera mahsusi na uratibu wa kikanda ili kufanikisha agenda hiyo muhimu kwa uchumi wa Afrika.
Mawaziri walioshiriki kikao hicho walikubaliana na Andiko hilo na kupendekeza hatua mbalimbali zifanyike ili Afrika iweze kutathmini maliasili zake.

Hatua hizo ni pamoja na umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja, kuwa na sauti moja hasa katika kuelekea mkutano wa kimataifa wa Mazingira COP29 utakaofanyika Baku, Azerbaijan Novemba 2024, kujengeana uwezo, ubia na utashi wa kisiasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news