Alphonce Simbu,Magdalena Shauri wawatoa jasho wanajeshi Afrika,waibuka vinara AMGA 2024

NA DIRAMAKINI

NOVEMBA 23,2024 Tanzania imefanya vizuri na kushinda katika mbio za kilomita 42 za Marathoni kwa wanaume na wanawake kwenye Michezo ya Kijeshi ya Afrika mwaka 2024 (AMGA 2024) inayoendelea jijini Abuja nchini Nigeria.
Mbio hizo zilikusanya wanariadha 100 kutoka Tanzania, Ethiopia, Uganda, Algeria,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ghana, Kenya, Libya, Afrika Kusini, Senegal na Nigeria ambaye ni mwenyeji.

Alphonce Simbu wa Tanzania alishinda wanaume kwa muda wa saa 2:17.19, huku akifuatwa na Dedefi Gelato wa Ethiopia alishika nafasi ya pili kwa kutumia saa 2:18.31. Laamedi El Hadi wa Algeria alimaliza katika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:19.59.
Magdalena Shauri wa Tanzania alishinda mbio za wanawake kwa muda wa saa 2:36.29, Cheptoyek Ruth na Chebet Emily wa Uganda walimaliza katika nafasi ya pili na ya tatu kwa muda wa saa 2:41.07 na 2:44.10 mtawalia.

Mbio zilianza saa 12:00 asubuhi kutoka lango la Jiji na kuelekea barabara ya uwanja wa ndege kabla ya kufanya mzunguko katika Uwanja wa Aco kwa kilomita 17.5.
Aidha, mbio ziliendelea kwa kilomita 21.19 kabla ya kufika katika Kituo cha Redio cha Nigeria (VON) na daraja la Kuchingoro kwa kilomita 30.5, kupitia Magic Land, Constitution Avenue hadi Churchgate kwa kilomita 37.5.

Baadaye, mbio ziligeuza kulia kwenye Barabara ya Olusegun Obasanjo na kuendelea hadi karibu na Hoteli ya Bolingo kabla ya kugeuka kwenye Barabara ya Kukwaba.

Mbio ziliendelea hadi Hospitali ya Taifa na kisha kuingia kwenye Uwanja wa Moshood Abiola National Stadium kwa kilomita 42.
Jumla ya michezo 20 inashindaniwa katika toleo la pili la AMGA 2024. Wanariadha zaidi ya 1,625 kutoka nchi 22 za Afrika wanashiriki kwenye michezo hii, ambayo ilifunguliwa Jumatano na inatarajiwa kumalizika Novemba 30,2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news