HARARE-Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-TROIKA), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amezisisitiza nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za kumaliza uhasama uliopo baina ya DRC na Rwanda chini ya mchakato wa Angola.
Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Dkt.Mwinyi kwa niaba ya Rais Dkt.Samia alipomwakilisha kufungua Mkutano wa Viongozi Wakuu na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika jijini Harare Zimbabwe tarehe 20 Novemba 2024.

Ameeleza kuwa, hatua hiyo itawezesha kupatikana kwa misaada ya kifedha na kilojistiki kwa wakati na kuongeza ufanisi wa Misheni za SADC na kupunguza gharama.