DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka Watoa Huduma za Mikopo Mitandaoni kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali katika utoaji wa huduma hiyo.
Akizungumza leo Novemba 14,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa semina kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini, Kaimu Meneja Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Bw. Dickson Gama amesema, Benki Kuu kwa kushirikiana na taaasisi zingine zimechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha watoa huduma hao wanafuata sheria zilizowekwa.
“Tunashirikiana na TCRA kuwafungia na kuwaondoa kwenye mtandao wanaofanya biashara hiyo bila leseni, lengo ni kuhakikisha kwamba kila anayetoa mikopo mitandaoni afuate sheria na taratibu zilizowekwa. Anayetoa mikopo mtandaoni pasipokuwa na leseni ni mhalifu."
Naye, Meneja Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Bi. Mary Ngassa, ameeleza kuwa,kufuatia changamoto ya ukiukwaji wa sheria katika utoaji wa mikopo kidijitali, Benki Kuu ilitoa 'Mwongozo kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili wanaotoa huduma za mikopo kwa njia ya kidijitali wa mwaka 2024’, mwezi Agosti 2024, ambapo Kifungu Na. 3.0 cha Mwongozo huo kimewataka watoa mikopo hao pamoja na mengine kuwa na leseni na kutunza faragha za wateja wao.
“Ili mtoa huduma ndogo za fedha kuruhusiwa kutoa mikopo kidijitali anatakiwa kuwa na leseni ya kuendesha biashara ya Huduma Ndogo za Fedha chini ya Daraja la 2 chini ya kifungu Na. 16 cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na awe amefuata matakwa ya Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Act) ya mwaka 2022 na kanuni zake."
Ameongeza kuwa, kufikia leo Novemba 14, 2024, Benki Kuu imepokea maombi 20 kutoka kwa watoa huduma hao na tayari taasisi nne zimeshapewa leseni ya kufanya biashara hiyo.
Kuhusu udhalilishaji wa wakopaji mtandaoni Meneja msaidizi huyo amesema, “Utaratibu ni kwamba mtu amekopa, hajalipa anapaswa kupewa notisi ya siku 14.
"Hajajibu anapewa siku saba na baada ya hapo unachukua hatua kwa utaratibu kwa kuchukua dhamana yake kwa njia ya kisheria, lakini wanapotishia watu na kuwadhalilisha ni kinyume na sheria na mteja unaweza kumshitaki.”
Kwa upande wa wahariri hao, wameishukuru Benki Kuu kwa kuendelea kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa makundi mbalimbali katika jamii na wameahidi kushirikiana na serikali katika kueneza elimu hiyo kwa wananchi.
Pia, amesema Benki Kuu inaendelea kuhuisha na kuchapisha orodha ya watoa huduma ndogo za fedha daraja la pili waliosajiliwa na kupewa leseni na Benki Kuu.
"Orodha hii inaonesha jina la taasisi, mahali ilipo, namba ya leseni, tarehe ya leseni,wamiliki na namba za mawasiliano."
Ngasa amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, Benki Kuu ya Tanzania imepewa jukumu la kusajili (kutoa leseni), kudhibiti na kusimamia taasisi za huduma ndogo za fedha nchini.
Amesema,sheria hiyo imegawa watoa huduma ndogo za fedha katika madaraja manne.
Daraja la kwanza linaundwa na taasisi za kibenki zinazotoa huduma ndogo za fedha (Microfinance Banks).
Pia, daraja la pili amesema, linaundwa na watoa huduma ndogo za fedha wasiopokea amana (non deposit taking Microfinance Service Provider).
Daraja la tatu amesema, linaundwa na vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (SACCOS) ambapo limekasimiwa kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC).
Kwa upande wa daraja la nne,amesema linaundwa na vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha (community microfinance group).
Amesema, daraja hilo la nne limekasimiwa kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).