Anzieni sokoni,malizieni shambani-Dkt.Serera

MOROGORO-Naibu Katibu Mkuu-Kilimo (Ushirika na Umwagiliaji), Dkt. Suleiman Serera amewataka Wakulima na Wanaushirika kuanzia sokoni na kumalizia shambani ili kujua mahitaji ya soko la mazao wanayotaka kulima na kuzalisha mazao kuendana na mahitaji ya soko.
Dkt. Serera ameyasema hayo Novemba 16, 2024 alipokuwa akiongea na wanaushirika wa UWAWAKUDA wakati wa ziara yake aliyoifanya kwenye Vyama vya Ushirika na Umwagiliaji vya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

"Wakulima wengi wanazalisha kile ambacho hakihitajiki sokoni; ni vizuri mkaanzia sokoni, mkamalizia shambani, bila kujua soko linataka nini hamuwezi kupata faida katika uzalishaji, mtaishia kulalamikia masoko," amesema Dkt. Serera.

Aidha, amewataka wakulima kuhakikisha kuwa wanazalisha mazao yenye ubora ili kuweza kupata uhakika wa kuuza mazao yao kwani soko la kimataifa linahitaji bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.

Kwa upande wake Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege amekipongeza Chama cha Ushirika cha UWAWAKUDA kwa kufanya kazi vizuri na kwa kufuata miongozo na kanuni za Vyama vya Ushirika katika kutekeleza majukumu yao.

Kutokana na ukosefu wa ghala la kuhifadhia mazao, Mrajis amekitaka Chama hicho kiweze kujenga ghala ambalo litakuwa msaada mkubwa kwa Wakulima na kurahisisha upatikanaji wa masoko.

Akitaja mikakati ya Chama, Mwenyekiti wa UWAWAKUDA, Charles Pangapanga, amesema kuwa moja ya mikakati waliyonayo ni kujenga ghala kubwa la kuhifadhia mazao na kuiomba Serikali kusaidia katika ujenzi wa ghala hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news