NA GODFREY NNKO
SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL) limeanza rasmi kutoa huduma zake tena kutoka Dar es Salaam hadi Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Hatua hiyo ya kihistoria imeanza tena leo asubuhi ya Novemba 30,2024 kwa kutumia ndege mpya ya B737-9 Max kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Walioshuhudia hafla hiyo ni Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. James Bwana, Balozi wa Tanzania, Afrika Kusini, Mhe. Balozi John Ulanga kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Makame Macharo Haji, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Prof. Neema Mori, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL pamoja na Mhandisi Peter Ulanga, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL.
ATCL ilisitisha rasmi safari zake kati ya Dar es Salaam na Johanessburg nchini Afrika Kusini, kuanzia Oktoba 7, 2019 ambapo abiria ambao walikuwa wamekata tiketi wakati huo kwa ajili ya usafiri huo walirudishiwa nauli zao.
Hayo yalibainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na ATCL Oktoba 3, 2019 na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo wakati huo, Ladislaus Matindi ikiwaelekeza mawakala wa tiketi wote kurejesha nauli za wateja hao ambao tayari walikuwa wamekata tiketi.
ATCL ambayo ilikuwa ikifanya safari hiyo mara nne kwa wiki kwa maana ya Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili iliacha kufanya safari kati ya miji hiyo Agosti 23,2019 baada ya ndege yake aina ya Airbus A220-300 kuzuiliwa katika Uwanja wa Oliver Tambo jijini Johannesburg kwa amri ya Mahakama Kuu ya Guateng.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya uchumi na masuala ya kidpolamsia wameikeza DIRAMAKINI kuwa,mafanikio hayo ya ATCL kurejesha huduma nchini Afrika Kusini yanatokana na matunda ya 4R za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Falsafa ya 4R za Rais Dkt.Samia inajikita katika masuala ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms) na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).