Baraza la Vyuo Vikuu vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (IUCEA) lakusudia kufungamanisha elimu ya juu

DAR-Baraza la Vyuo Vikuu vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (IUCEA) limekutana na Wadau pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ili kutoa mafunzo mbalimbali ambayo yatahusika katika ufungamanishaji wa elimu ya juu katika ukanda huo na kuwaeleza wadau juu ya fursa mbalimbali katika jumuiya hiyo.
Akizungumza Novemba 20, 2024 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema katika jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kwa pamoja kufungamanishwa Elimu ya juu ili kuondoa tofauti kwa elimu inayotolewa katika ukanda huo.

Aidha Prof. Nombo amesema makubaliano ya hatua hiyo yatafungua fursa kwa wanafunzi katika Jumuiya hiyo kuweza kusoma katika nchi nyingine pamoja na kubadilishana wataalam.

Ameeleza kuwa, IUCEA imeangalia mambo mbalimbali ikiwemo suala la mitaala, ada katika vyuo ili kutimiza nia yao ya kufungamanisha suala la elimu katika Jumuiya ambapo itafungua fursa kwa wanafunzi wa Tanzania, Kenya, Uganda na sehemu zingine katika Jumuiya kwenda kusoma nchi anayotaka.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shahada za uzamili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Donata Damian amesema mkutano huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga ufahamu namna ambavyo wanafunzi wanaweza kwenda katika vyuo vingine katika Jumuiya hiyo na namna ambavyo itafungua mwanya kwa wanafunzi wengine kuja kusoma nchini.

Aidha, Prof. Donata ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo yatawezesha kuondoa vikwazo ambavyo vilizuia wanafunzi kutoka sehemu moja ya Jumuiya kuja nchini kwa ajili ya kusoma kutokana na kutofautiana kwa mitaala.

"Ulinganifu wa elimu yetu ya sekondari unatofautiana, ukiangalia Kenya hawana kidato cha tano na sita, akija hapa kwetu tuwezeje kumshirikisha aingie katika vyuo vyetu,'' amesema.

Naye Mtendaji Mkuu IUCEA Uganda, Prof. Gasper Kibona amesema IUCEA imeboresha masuala mbalimbali ya sera, pamoja na miongozo ya viwango vinavyotakiwa ambapo baada ya kukamilisha sera hizo walizisambaza kwa wadau.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news