DAR-Bodi ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania (TPLB) imethibitisha kupokea barua ya Young Africans Sports Club ya kuomba kuutumia uwanja wa KMC CComplex jijini Dar es Salaam.
Ni kwa michezo yake ya nyumbani badala ya Azam Complex ambako walikuwa wanautumia awali ingawa ombi hilo bado halijatolewa majibu hadi sasa.
Afisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda amesema,ombi la Yanga SC linaangukia kwenye Kanuni ya 9 ya TPLB inayotoa ruhusa kwa klabu ambayo haina uwanja wa nyumbani kuchagua uwanja mwingine ambao utakuwa ndani ya mkoa ule ule ambao walikuwa wanacheza ama mkoa wa jirani ilimradi uwe unakidhi vigezo.
“Barua ambayo Young Africans Sports Club wameiandikia Bodi ya Ligi inaeleza kuwa klabu hiyo haina uwanja, wameshamalizana na wamiliki wa uwanja wa Azam Complex, Chamazi kwa hiyo wanakwenda kuangukia kwenye hiyo kanuni ya 9 Ibara ya 4.”