MWANZA-Waandishi wa habari wameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kuwa miongoni mwa taasisi za umma ambazo ziko mstari wa mbele katika kufanya kazi na makundi mbalimbali katika jamii, wakiwemo waandishi wa habari.
Waandishi hao wa habari wamesema hivyo katika maazimio yao waliyotoa mwishoni mwa semina iliyoandaliwa na Benki Kuu kwa ajili ya waandishi wa Kanda ya Ziwa wakiwa kutoka mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Kagera na Mara.
“Benki Kuu ni taasisi ya mfano iliyo mstari wa mbele kwa kutambua na kufanya kazi na waandishi wa habari,” amesema Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Mwanza, Bw. Edwin Soko na kuitaka iendelee kuwajengea uwezo waandishi wa habari na tasnia zingine.
Akifunga mafunzo hayo, Meneja Uendeshaji wa tawi la Benki Kuu Mwanza, Bi. Zainabu Amasi, amewashukuru waandishi hao 36 wa Kanda ya Ziwa kwa kuitikia mwito wa kushiriki katika semina hiyo ya siku mbili na kuwataka kuendelea kuonesha ushirikiano na Benki kila wakati.
“Tunaomba sisi kama uongozi wa Benki Kuu tuzidi kushirikiana, hata pale mnapolisikia jambo lolote lile, sisi milango yetu iko wazi…Ninyi ndio wa kutusemea; kalamu zenu zina nguvu zaidi pamoja na ndimi zenu zina nguvu zaidi,” alieleza Bi. Amasi.
Aidha, ameeleza kufurahishwa kwake kwa waandishi hao wa habari kupata mada inayoelezea uamuzi wa kuondoa pesa za zamani kwenye mzunguko.
“Jambo la uondoaji hizi pesa kwenye mzunguko limeanzia kwenu, na kutoka hapa sasa sisi tutakwenda kwa wananchi lakini ni ninyi pia mtakuwa wawakilishi wetu huko kwa wananchi kuweza kuzungumzia yote mliyoyapata,” amesema Meneja Uendeshaji.
Ameeleza matumaini yake kwamba mambo ambayo waandishi hao wa habari wamejifunza yamewapa uelewa zaidi na kwamba wataweza kuyaelezea vizuri zaidi kupitia vyombo vyao vya habari.
“Nina matumaini kuwa mambo yote mliyojifunza hapa, mmetoka mmekuwa walimu wazuri, mmejua majukumu ya Benki Kuu ya Tanzania kwa undani…kwamba kazi ya Benki Kuu kumbe si usambazaji wa sarafu na utengenezaji wa sarafu tu, mambo ni mengi na hapa mmepata sehemu tu,” amesema.
Waandishi hao wa habari walipata pia mada kuhusu umuhimu wa ununuzi wa dhahabu, mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na kanuni zake, kutambua alama za usalama wa fedha zetu pamoja na namna bora ya kutunza pesa zetu ili zisichakae haraka.