DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo kwa wafanyakazi wa benki za biashara jijini Dodoma kuhusu zoezi la kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani, linalotarajiwa kuanza rasmi tarehe 6 Januari hadi 5 Aprili 2025.
Mafunzo hayo yaliyotolewa na Meneja Uendeshaji kutoka Tawi la BoT Dodoma, Bw. Nolasco Maluli, yametoa fursa kwa washiriki kujifunza kwa vitendo alama za usalama zilizopo katika noti hizo pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia katika utekelezaji wa zoezi hili muhimu.
Noti za zamani zitakazoondolewa kwenye mzunguko ni pamoja na shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1000), elfu mbili (2000), elfu tano (5000) na elfu kumi (10000) kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003, na noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010 zenye sifa zilizoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 858 la tarehe 11 Oktoba 2024.
Matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania kuanzia tarehe 06 Aprili, 2025. Baada ya tarehe hiyo, mtu yeyote au taasisi yoyote inayomiliki fedha hizo haitaruhusiwa kuzitumia katika kufanya malipoi; na benki zote hazitaruhusiwa kulipa wala kupokea amana au maombi ya kubadilisha noti zilizoondolewa kwenye mzunguko.
Vilevile, zoezi hili litafanyika kupitia Ofisi za Benki Kuu na Benki za Biashara nchini ambapo mwananchi atapatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi alichowasilisha.