DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetembelea Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC-UDSM) kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa chuo hicho kuhusiana na majukumu yake.
Katika mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 22 Novemba, 2024, washiriki walipata fursa ya kujifunza namna Benki Kuu inavyoandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.
Pia, wameelimishwa kuhusu jukumu la Benki la Kuu la kutengeneza na kutoa fedha (noti na sarafu) kwa matumizi nchini.
Aidha, wameelezwa kuhusu zoezi la kuondoa katika mzunguko noti za zamani za shilingi ishirini 20, 200, 500, 1000, 2000, 5000 na noti za shilingi 10000. Noti hizo zinazoondolewa ni za matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003, na noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010. Zoezi hilo linatarajiwa kuanza tarehe 6 Januari 2025 hadi 5 Aprili 2025.
Kwa upande wake, Amidi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari (SJMC-UDSM), Dkt. Mona Mwakalinga, ameishukuru Benki Kuu kwa kuwajengea uwezo wanafunzi hao kuhusu masuala ya uchumi na fedha na kwa kutambua umuhimu wa sekta ya habari katika kuendeleza uchumi wa nchi.
Naye kiongozi wa ujumbe wa Benki Kuu, Meneja Msaidizi Idara ya Utafiti, Dkt. Lusajo Mwankemwa ameishukuru Shule hiyo kwa kutoa fursa hiyo ya mafunzo na kuahidi kwamba Benki Kuu itakuwa tayari kushirikiana na shule hiyo ili kukuza uelewa wa wanafunzi wa uandishi wa habari kuhusu masuala yanayohusu sekta ya fedha, eneo ambalo Benki Kuu inasimamia.